Ndugu, Natumaini umewahi kununua viatu, nguo au mahitaji madogo madogo ya nyumbani kama vile sukari, chumvi au chakula. Je, ulipomaliza kutumia mahitaji hayo, ulikuwa ni mwisho wa maisha yako? Jibu ni hapana. Uliendelea kuyanunua tena na tena, maana ni muhimu katika kuendesha maisha yako.
Kwa kuwa ni muhimu, basi kuna sehemu unaenda mara nyingi kuchukua mahitaji hayo. Huendi kwa sababu wanayo bali kuna namna unapata huduma nzuri.
Kama muuzaji au mhudumiaji kumuuzia mteja mara moja ni hasara. Hii ni kwa sababu umetumia muda, gharama kumfanya anunue kwako. Suala muhimu ni kumbakiza katika huduma yako. Pamoja na njia mbalimbali zilizopo katika kumbakiza mteja, leo tunaenda kuangalia mojawapo kama ilivyoelezewa hapa chini;
Kukaa Kwenye Mchakato
Kuna wakati nawaza, kama mauzo yangekuwa kwamba unakutana na mteja unazungumza naye dakika moja ananunua basi tungekuwa na pesa nyingi sana. Kusingekuwa na haja ya kuandaa makala kama hizi zinazoelezea mbinu za kuuza zaidi au kuongeza ushawishi kwa wateja.
Masuala ya mafunzo, semina yasingeweza kufanya kazi. Lakini kwa kuwa siyo hivyo basi kuna mchakato unaopaswa kuupitia ili kuwa karibu na kuendelea kumuhudumia mteja.
Mauzo nayafananisha kama mapenzi. Huwezi kumuona Binti leo, ukamtongoza leo akakubali na ukamuoa leo leo. Ikitokea itakuwa moja ya maajabu ya Dunia. Utatakiwa kujengewa sanamu, maana umekuwa wa kwanza kufanya jambo ambao halijawahi kutokea.
Lakini mara nyingi kuna mchakato inabidi ufuate mpaka kufikia maelewano na binti huyo hadi unamuoa. Masuala ya kuwasiliana, kuonana naye na zawadi za mara kwa mara ndivyo hukupa nafasi ya kumbakiza kwako.
Tunapokuwa katika mauzo namna nzuri kuyafanikisha ni kukaa kwenye mchakato sahihi kwa sababu “Mauzo sio tukio, bali ni mchakato”. Ni zoezi endelevu ambalo halina mwisho. Linahitaji ufuatiliaji wa karibu sana kuhakikisha mteja anaelewa vema biashara yako.
Mfano mwingine unaoweza kuutumia kuelewa mauzo ni kulinganisha na daladala, ambapo kila wakati kuna abiria wanapanda na wengine wanashuka. Kondakta wa daladala hakubali gari lake liende likiwa tupu. Abiria wanaposhuka anatafuta wengine wa kujaza sehemu zilizoachwa wazi.
Kondakta hawasemi kwa kuwa abiria alishailipia nafasi basi twende tu hivyo hivyo hadi mwisho badala yake wanakazana kutafuta abiria wengine. Pengine hata wewe mwenyewe baada ya kushuka wanakuuliza au kukuita tena kwenye gari. Wanaamini unaweza kuwa umeshuka sehemu sio au kubadili maamuzi.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuendesha mchakato wako wa mauzo, kila wakati unapaswa kuwa umejaza nafasi. Nafasi za wateja tarajiwa uliowapata na unaoendelea kujenga nao mahusiano na kuwashawishi kununua. Pale mteja anapokamilisha mauzo kwa maana ya kulipia bidhaa yako, nafasi yake inapaswa kuchukuliwa na mteja tarajiwa mwingine ambaye utaendelea kumchakata mpaka anunue.
Hata baada ya mteja kununua kwa maana ya kukamilisha mauzo, sio mwisho wake wa kumfuatilia. Badala yake unahitaji kumrudisha tena kwenye mchakato ili aweze kununua zaidi. Na hata kama sio yeye atakayenunua, basi unaweza kumtumia kupata wengine kupitia yeye watakaonunua zaidi.
Unaweza kuona jinsi gani mauzo yalivyo mchakato na sio tukio, hufanyi kitu chochote mara moja, bali unakifanya kwa mwendelezo. Ili kukamilisha mchakato huu wa mauzo, lazima uwe na mfumo mzuri wa kuwasiliana na wateja wako kama nilivyoelezea katika masomo yaliyopita. Kuhakikisha taarifa zao unazitunza vizuri ili uwafanye waendelee kubakia katika biashara au huduma yako.
Hivyo wajibu wako ni kuwaweka kwenye mchakato, kwenda nao mara zote. Huku ukiwasaidia zaidi pale wanapohitaji huduma yako. Ukiweza kujijengea mtazamo wa kuchukulia mauzo kama mchakato na sio tukio, utaweza kukaa kwenye mchakato sahihi ambao utakupa manufaa makubwa. Maana unapopoteza mteja mmoja, huoni ndiyo mwisho wa mauzo, badala yake unachukulia kama fursa ya kupata wateja zaidi ambao utaendelea kuwachakata na kuwabakiza katika biashara yako.
Je, umeweka mfumo au utaratibu upi wa kuwabakiza wateja katika biashara yako?
Habari njema ni kuwa, kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA kipo jikoni kinaandaliwa. Unawabakizaje wateja katika biashara yako na mengine. Vyote vipo ndani ya kitabu hicho. Endelea kutufuatilia hapa hapa ili uwe wa kwanza kupata kitabu hicho pindi kitakapokuwa tayari.
Imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata makala na kitabu.
Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi.
Hide comments