Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Uwezo mkubwa ulio ndani yako wa kufanya makubwa.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora. Hiyo ni kwa sababu jinsi unavyofanya kitu chochote kwenye maisha, ndivyo unavyofanya kila kitu. Huwezi kukazana kuwa bora kwenye mauzo kama kwenye maeneo mengine siyo bora.

Uzuri ni kwamba, huhitaji kutafuta ubora na kuuweka ndani yako. Tayari ubora upo ndani yako, ni wewe tu hujaweza kuufikia na kuutumia ubora huo kufanya makubwa.

Kila binadamu aliye hai, anao uwezo mkubwa ndani yake kuliko ambavyo anautumia. Uwezo huo upo kwenye kila eneo la maisha. Chochote unachotumia sasa, ni kidogo sana ukilinganisha na kilichopo.

Maisha yetu ya kawaida huwa hayahitaji mtu utumie uwezo mkubwa. Kwani kwa kufanya tu mambo ya kawaida, maisha yanaweza kwenda.

Lakini kufanya mambo ya kawaida ni kikwazo kwa mtu kupata matokeo ya tofauti na yatakayompa mafanikio makubwa. Watu wengi hawafanikiwi siyo kwa sababu hawana uwezo wa kufanikiwa, bali kwa sababu hawajatumia uwezo mkubwa walionao.

Na hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mauzo. Kila mtu tayari anao uwezo wa kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea. Kinachowazuia wengi wasifikie huo uwezo wa kuwa wauzaji bora ni kuendelea kuyaishi maisha yao kwa mazoea. Wanakuwa wanafanya yale waliyozoea kufanya mara zote. Hawajifunzi wala kujaribu vitu vipya.

Kudhihirisha hili kwako mwenyewe, kumbuka wakati ambao ulilazimika kufanya kitu ambacho ulikuwa unadhani huwezi kufanya. Labda ni kukimbizwa na mnyama mkali na ukajikuta umeruka ukuta ambao katika hali ya kawaida usingeweza kuuruka. Au pale ulipokuwa na mahitaji makubwa sana kiasi cha kupata msukumo mkubwa wa kufanya kila kinachohitajika ili uweze kukamilisha mahitaji hayo.

Kwa mifano hiyo na mingine mingi uliyonayo kwenye maisha ni kiashiria tosha kwamba uwezo mkubwa tayari unao, ni wewe tu unakwama kuutumia. Ukiweza kutumia uwezo mkubwa ambao tayari upo ndani yako, utaweza kufanya makubwa zaidi ya unavyofanya sasa.

Kutumia uwezo mkubwa ambao tayari upo ndani yako ili kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, zingatia haya;

Moja; toka nje ya mazoea.

Hakuna kinachokukwamisha kama kufanya vitu kwa mazoea. Anza kwa kutoka nje ya mazoea. Na hilo linaanzia kwenye malengo unayojiwekea. Umekuwa unaweka malengo kwa kufikiria nini unaweza kufikia. Na hilo linakurudisha kwenye mazoea.

Malengo sahihi kwako kuweka ambayo yatakutoa kwenye mazoea ni kuchukua malengo unayoona unaweza kuyafikia na kuzidisha mara 10. Hayo ndiyo yanakuwa malengo yako mapya. Malengo hayo mapya makubwa na makubwa yatakutisha sana, lakini hupaswi kuyaogopa, kwani uwezo wa kuyafikia tayari unayo.

Mbili; chukua hatua kubwa zaidi.

Kuweka malengo makubwa ni hatua moja, hatua nyingine ambayo ni muhimu zaidi ni kuchukua hatua kubwa kwenye malengo makubwa uliyojiwekea. Fanya zaidi ya ulivyozoea kufanya. Fanya kwa wingi na ukubwa ili uweze kuzalisha matokeo ya tofauti.

Kwenye kuchukua hatua kubwa usikubali kulaghaiwa na mwili wako. Mwili wako huwa unafanya kazi ya kukudanganya ili usiuchoshe. Hivyo unakuonyesha kwamba umechoka na huwezi kuendelea tena. Lakini unapokuwa umefikia hiyo hatua ya kuona umechoka na huwezi tena, jua hujafika hata nusu ya uwezo wako wa kuendelea kufanya.

Unachohitaji ni kuendelea kujisukuma kufanya hata kama unaona umeshafanya sana. Unao uwezo wa kuendelea kufanya zaidi ya vile unavyokuwa umeshafanya.

Tatu; zungukwa na watu sahihi.

Tunaujua usemi kwamba wewe ni wastani wa watu watano unaokuwa nao kwa muda mwingi. Hivyo mafanikio yako kwenye mauzo yatategemea sana mafanikio ya wale wanaokuzunguka.

Kama umezungukwa na watu ambao wanakazana kuwa bora, na wewe pia utapata msukumo wa kuwa bora. Na kama umezungukwa na watu walioshindwa, na wewe pia utashindwa.

Watu wanaokuzunguka wana nguvu kubwa ya ushawishi kwako. Hao ndiyo watakaoamua ni mafanikio kiasi gani uyapate, kulingana na mafanikio ambao nao wanayapata.

Chagua watu sahihi ambao watakupa msukumo wa kupiga hatua kubwa zaidi kwenye maisha yako. Jifunze kwa wale ambao wameshafika pale unakotaka kufika na jua kama wao wameweza kufika, na wewe pia unaweza kufika.

Kuliko kutumia muda wako na watu walioshindwa na kukata tamaa ni bora ubaki ukiwa mpweke na kuyapambania malengo yako.

Ishi kwenye hayo matatu mara zote kwa kuwa na malengo makubwa, kuchukua hatua kubwa na kuzungukwa na watu sahihi. Ni kwa njia hiyo ndiyo unaweza kuwa mtu bora na hatimaye kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea. Yote hayo hapo ndani ya uwezo wako, ni wewe kupanga na kuchukua hatua.

Usikubali kuishi maisha ya kawaida na kuacha uwezo mkubwa ukiwa umelala ndani yako. Fikia na tumia uwezo huo ili kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora. Kocha Dr. Makirita Amani, Mkuu wa CHUO CHA MAUZO www.mauzo.tz

1 Comment

  • Miraji abdallah
    Posted November 13, 2023 at 8:07 pm

    Ili niwe muuzaji bora ninapaswa kwanza Mimi ni Bora.
    _tayari ninaumwezo wa kunifanya niwe Bora ni Mimi tu kuufikia na kutumia
    _ nitajisukuma kuepuka kufanya biashara kwa mazoea.
    _nitayaepuka mazoea kwa kuweza Marengo Mara kumi ya vile ninavyoweka Sasa na pia nitachukua hatua kikamilifu.

    Asante Sana kocha

Leave a comment