Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora. Ni ubora wako kwenye kila eneo la maisha yako ndiyo utakaokuwa na mchango kwenye mafanikio yako kimauzo.
Tunafanya yale tunayoyafanya kwa sababu kuna vitu tunavyotaka kupata kwenye maisha yetu. Kupata tunachotaka ndiyo msukumo mkubwa kwa kila mmoja wetu kufanya yale anayofanya.
Kwa upande wa pili, chochote kile tunachotaka, watu wengine ndiyo wanacho. Hivyo ili kupata tunachotaka, tunahitaji watu wengine watupe. Na hapo ndipo penye siri kuu ya kupata chochote unachotaka, ambayo watu wamekuwa wakiipuuza.
Kwa sababu unachotaka wanacho wengine, kuna njia mbili za kukipata.
Njia ya kwanza ni kuwalazimisha wakupe. Hapa unaweza kufanya hivyo kwa kuwaibia, kuwadhulumu, kuwadanganya na njia nyingine za aina hiyo. Njia hii inaweza kukupa unachotaka kwa haraka, lakini ni njia ambayo huwa haidumu, kwani mwisho wake huwa ni mfupi.
Njia ya pili ni kuwashawishi wakupe wao wenyewe. Hapa unawafanya watu, kwa ridhaa yao wenyewe wakupe kile walichonacho. Tena wafurahie kufanya hivyo. Njia hii inaweza kuchukua muda mrefu kukupa unachotaka, lakini ni njia ya uhakika na isiyo na ukomo. Kwa sababu watu wakishakuwa tayari kukupa unachotaka, wataendelea kukupa zaidi na zaidi.
Kinachowakwamisha wengi kwenye maisha ni kushindwa kuwashawishi watu wawape kwa ridhaa yao wenyewe, kile wanachotaka. Na hiyo ni kwa sababu wanapuuza sheria hii muhimu sana ya kupata chochote unachotaka. Sheria hiyo inasema; KUPATA CHOCHOTE UNACHOTAKA KWENYE MAISHA YAKO, WAPE WATU WENGI ZAIDI KILE WANACHOTAKA.
Kwenye hiyo siri kuna mambo mawili ambayo tutayawekea msisitizo mkubwa, hasa kwenye upande wa mauzo. WAPE WATU WANACHOTAKA na WAPE WENGI ZAIDI.
Lakini kabla ya kuingia kwenye msisitizo wa hilo, turudi kwenye asili ya binadamu na kwa nini hii sheria inafanya kazi. Kwa asili sisi binadamu ni wabinafsi, huwa tunaweka maslahi yetu mbele kabla ya maslahi ya wengine. Kwenye kila jambo tunalojihusisha nalo, swali la kwanza tunalojiuliza ni NAPATA NINI HAPA?
Ili ufanikiwe, hupaswi kwenda kinyume na asili ya binadamu, badala yake unapaswa kuifuata. Sasa kwa sababu watu wanaangalia wanapata nini, ili wakupe unachotaka, anza kwa kuwapa kile wanachotaka. Kabla hujamwambia mtu akupe, anza wewe kumpa. Pale mtu anapoona anapata anachotaka, ndiyo anakuwa tayari kutoa kile anachopaswa kutoa.
Sasa turudi kwenye mambo mawili makubwa ya kuzingatia ili kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea.
Anza kwa KUJUA AMBACHO WATU WANATAKA.
Kwa chochote unachouza, jua watu hawanunui kwa sababu wewe unauza, bali wananunua kwa sababu zao binafsi. Hivyo ili uwe muuzaji bora, usiangalie tu unauza nini, bali angalia watu wanataka nini kwenye kile unachouza.
Hili ni muhimu sana, kwa sababu unaweza kukazana sana kuwaambia watu wanunue, kwa sababu unataka kuuza. Lakini hawatajali kama hawaoni wakipata kile wanachotaka. Kwa kujua kile ambacho watu wanataka na kuwaonyesha wanaweza kukipata kwa kununua unachouza, unakuwa umerahisisha kazi.
Swali ambalo unaweza kujiuliza ni utajuaje kile watu wanachotaka? Jibu ni rahisi, waulize, wasikilize na waangalie. Majibu yapo wazi kama utataka kuyapata.
Kisha nenda kwenye KUWAPA WENGI ZAIDI WANACHOTAKA. Baada ya kujua watu wanataka nini kwenye kile unachouza, kazi kubwa inayokuwa imebaki kwako ni kutafuta watu wengi zaidi wenye kutaka kitu hicho na kuwapatia.
Kwa wale uliojua wanachotaka kwenye kile unachouza, kuna sifa ambazo wanazo. Kazi yako ni kuwatafuta wengi zaidi wenye sifa za aina hiyo na kuwapa hicho wanachotaka. Kadiri unavyowapa wengi zaidi kile wanachotaka, ndivyo unavyofanya mauzo makubwa zaidi na kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea.
Wewe kuwa muuzaji bora haianzii na kile unachouza. Ndiyo maana kuna watu huwa wanahangaika kubadili wanachouza kila mara, kwa kwenda na mkumbo, lakini bado hawafanikiwi. Wewe kuwa muuzaji bora kunaanza na kuwajua vizuri watu, kile wanachotaka na kuweza kuwapa kwa namna ambayo hawapati mahali pengine. Kisha kufanya hivyo kwa wengi zaidi.
Swali muhimu sana la kuondoka nalo hapa ni watu wanataka nini hasa kwenye hicho unachouza? Hili ni swali ambalo unapaswa kuwa na majibu yake kwa uhakika na kuwa unayafanyia kazi mara zote.
Ukishajibu swali la watu wanataka nini, swali jingine utakaloendelea nalo ni unawezaje kuwapa wengi zaidi hicho wanachotaka.
Haya siyo maswali ya kujibu mara moja na kwenda kwa mazoea. Bali ni maswali ya kujiuliza na kujijibu kila siku, kwa sababu mambo yanabadilika. Matakwa ya watu yanabadilika, hivyo lazima na wewe uende ukibadilika. Pia watu wanabadilika, waliopo wanaondoka na wapya wanakuja, hivyo kila mara lazima uwe unawafikia wapya wengi zaidi.
Ishi kwa kanuni hii ya kuwapa wengi zaidi kile wanachotaka ili na wewe uweze kupata kile unachotaka. Hivyo ndivyo utakavyoweza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora. Kocha Dr. Makirita Amani, Mkuu wa CHUO CHA MAUZO www.mauzo.tz