Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Ndoto, Malengo na Mipango.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora.
Ni ubora wako kwenye kila eneo la maisha yako ndiyo utakaokuwa na mchango kwenye mafanikio yako kimauzo.

Ubora wako binafsi unapimwa na matokeo unayozalisha kwenye maisha yako, ambayo ni mafanikio unayokuwa unayapata kwenye kitu chochote unachofanya.

Watu wengi wamekuwa wanataka kupata mafanikio, lakini wamekuwa wanakwama, kwa sababu hawachukui hatua zilizo sahihi kwao kupata mafanikio wanayokuwa wanayataka.

Kosa la kwanza ambalo wengi wanaanza nalo ni kukimbizana na mafanikio ambayo siyo yao, bali ya watu wengine.
Yaani wanahangaika na mambo wanayoona yatawapa mafanikio, lakini hata wakipata mafanikio hayo bado wanakosa ridhiko la ndani.
Hiyo ni kwa sababu wanakuwa wamehangaika na mambo yenye tija kwa wengine ila siyo kwao.

Ili kujenga mafanikio yenye tija kwako, unapaswa kufuata ngazi hizi tatu muhimu; Ndoto, Malengo na Mipango.

Ngazi ya kwanza ni ya ndoto kubwa unazokuwa nazo ndani yako.
Hii ni picha unayoiona kwenye fikra zako ya vile unavyotaka maisha yako yawe.
Picha hii inaanzia ndani yako mwenyewe na haitokani na picha za wengine.
Hii ni namna unavyojiona wewe mwenyewe ukiyaendesha maisha yako kwa namna ambayo unaridhika.

Kila mtu aliye hai ana ndoto kubwa za maisha yake, ambazo zinatofautiana kabisa na za watu wengine.
Kwa bahati mbaya sana, wengi wamekuwa wanakosa uthubutu wa kuziishi ndoto kubwa wanazokuwa nazo kwa sababu hazifanani na za wengine au ni za tofauti na ambazo hazijazoeleka.

Wewe usikubali kuzima ndoto zilizo ndani yako kwa sababu tu hakuna mwingine anayeziona.
Kuna sababu kwa nini ni wewe tu unayeweza kuziona ndoto hizo kubwa ulizonazo.
Ni kwa sababu ipo ndani ya uwezo wako kuzitimiza ndoto hizo.

Kuwa na ndoto ni ngazi ya kwanza na muhimu kwenye kujenga mafanikio makubwa. Lakini ndoto hizo hazitakamilika tu kimiujiza kwa sababu unataka sana zikamilike.

Ngazi ya pili ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha ni kuwa na malengo.
Hapa pia ndipo wengi wamekuwa wanapotea, kwa kujikuta wanahangaika na malengo ambayo siyo sahihi kwao.
Watu wamekuwa wanaiga malengo ya wengine, kwa kudhani hayo ndiyo sahihi zaidi.
Malengo sahihi kwako ni yale yanayokupeleka kwenye ndoto kubwa unazokuwa nazo.
Malengo unayokuwa nayo yanatakiwa yatokane na ndoto kubwa unazokuwa nazo na siyo vinginevyo.

Kwa kuanza na ndoto kubwa, kisha kuweka malengo ambayo ndiyo yanakufikisha kwenye ndoto hizo yanakuwa ni malengo sahihi kwako kufanyia kazi.
Usiwe na malengo ya kuiga au kufuata mkumbo, bali jua jinsi ambavyo kila malengo uliyonayo yanachangia wewe kufikia ndoto kubwa ulizonazo.
Kama una lengo lolote ambalo halina mchango kwako kufikia ndoto zako, siyo lengo sahihi kwako, bali ni usumbufu kwako.

Ndoto ni kule unakotaka kufika, malengo ni safari ya kufika huko. Hapo kuna kitu muhimu kinachokuwa kinahitajika ili kufika unakoelekea, ambacho ni kukaa kwenye safari yenyewe.

Ngazi ya tatu ya kupata mafanikio makubwa ni kuwa na mipango.
Mipango ni utekelezaji wa malengo ambayo mtu unakuwa nayo.
Ni hatua ambazo mtu unachukua ili uweze kufika kule unakotaka kufika.
Mipango ndiyo inaamua nini unafanya na unafanyaje ili kufikia malengo na kutimiza ndoto unazokuwa nazo.

Mipango ndiyo safari yenyewe, ambayo inahusisha mambo mbalimbali yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kutekeleza malengo na kuzifikia ndoto.
Mipango ni aina ya maisha ambayo mtu unachagua kuyaishi ambayo yanaweka vipaumbele kwenye yale yaliyo ya msingi kabisa na kuondokana na usumbufu mwingine mwingi.

Bila ya kuwa na mipango kila kitu kinaweza kuonekana ni muhimu, wakati vingi siyo muhimu.
Vitu vingi vinavyowinda muda na umakini wako wa kila siku havina umuhimu mkubwa.
Lakini hutaweza kujua hilo kama hujaweka mipango ya mambo gani unayofanya kila siku ili kufikia malengo uliyonayo.

Wengi wamekuwa wanaweka malengo bila ya mipango na kushangaa kwa nini hawayafikii malengo hayo.
Malengo bila ya mipango thabiti ya kuyafikia yanabaki kuwa matamanio tu.
Matamanio wengi wanayo na hayajawasaidia.
Kitakachokusaidia wewe ni mipango unayokuwa nayo na utekelezaji wake.

Jinsi ya kutumia haya kwenye mauzo.

Ili kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, unapaswa kutumia ngazi hizo tatu za Ndoto, Malengo na Mipango.

Unaanza na ndoto kubwa ulizonazo kwenye maisha yako, kisha kuziunganisha na mauzo.
Kwa kuwa ndoto hizo zinaendana na vitu fulani unavyopenda au kuweza zaidi, unapaswa kujiuliza nini unapaswa kuuza na watu gani unaopaswa kuwauzia ndiyo uweze kufikia ndoto kubwa unazokuwa nazo.
Anza na ndoto kubwa ulizonazo ili kujua kipi sahihi kwako kuuza ili kuzifikia.
Hata kama siyo kile unachouza sasa, kujua itakusaidia kukua kwenye huo uelekeo.

Kinachofuata ni kuweka malengo ya kuzifikia ndoto kubwa ulizonazo kupitia uuzaji.
Ndoto zimeshakuongoza uuze NINI na kwa NANI.
Malengo yanakuongoza uuze kwa ukubwa kiasi gani ili kuweza kuzifikia ndoto.
Hii ni hesabu utakayoifanya kulingana na ndoto ulizonazo na kile unachouza.
Lakini ni muhimu uwe na malengo yanayokuongoza kwenye ufanyaji.

Mipango ni hatua za utekelezaji wa malengo ya mauzo uliyoweka.
Ukubwa wa mauzo unaopaswa kufanya ili kufikia ndoto kubwa ulizonazo unapaswa kuugawa kwenye mipango ya utekelezaji.
Mipango inahusisha wateja wangapi uwe nao na kila mteja anunue kiasi gani ili ufikie malengo uliyojiwekea.
Namba hizo ndizo utakazofanyia kazi kila siku ili kutimiza ndoto kubwa unazokuwa nazo.

Hivyo ndivyo unavyoweza kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, kwa kuongozwa na ndoto kubwa ulizonazo, unazoziwekea malengo ya kuzifikia na hatua za kufanyia kazi kila siku ili kuyafikia.
Ukikaa kwenye huo mchakato kwa msimamo bila kuacha utaweza kupata mafanikio makubwa kadiri ya unavyotaka.

Tumia Ndoto, Malengo na Mipango kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea na itakuwa na manufaa kwako na kwa wengine pia.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora.
Kocha Dr. Makirita Amani,
Mkuu wa CHUO CHA MAUZO
www.mauzo.tz

Leave a comment