Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Leo ikiwa ni jumamosi ya ushawishi, tunaongozwa na kauli mbiu ya ushawishi inayosema, HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Ili tupate vitu ambavyo hatuna tunahitaji kuwashawishi watu waweze kukubaliana na sisi. Hakuna kitu ambacho tunaweza kupata kwenye maisha bila kuwashawishi wengine.
Kama tulivyoona kwenye silaha mbili tulizojifunza silaha ya ushawishi ya fadhila na dhamira na msimamo jinsi inavyofanya kazi.
Sisi binadamu ni viumbe vya kijamii, hivyo basi huwa tunaathiriwa sana na kile ambacho wengine wanafanya.
Tunapoona kundi kubwa la watu linafanya kitu fulani, basi huwa tunaamini hicho ni kitu sahihi kufanya na tunajikuta na sisi kushawishika kufanya pia.
Kwa mfano, kuna kauli ambazo jamii huwa inatumia kuhalalisha kwamba kile walichosema ni wengi ndiyo sahihi. Kwa mfano, kauli kama vile; wengi wape, penye wengi hapaharibiki neno.
Kwenye jamii, ukweli huwa unaoonekana pale walipo wengi.
Hata wewe ukienda ugenini, ukiwa hujui nini ufanye huwa unafanya kile ambacho huwa kinafanywa na wengi. Na utaamini kwamba ni sahihi hata kama siyo sahihi.
Kwenye maisha vitu vingi ambavyo watu wanafanya vingi wanaiga. Kwa kuthibitisha hili, kuliwahi kufanyika utafiti na mkufunzi wa mauzo na kusema kwamba, asilimia 5 ya watu ndiyo wanaofanya ubunifu na wengine wote 95 asilimia wanaiga.
Watu wanaigana kwenye kununua, viatu, nguo, viwanja, ramani za nyumba zinazofanana, magari, simu watu huwa wakipenda kitu watakuambia na mimi nataka kama ya fulani.
Kazi yetu kubwa ni kuitumia hii silaha ya ushawishi, kuweza kuwashawishi wateja wetu kuweza kukubaliana na sisi kisha kuwashawishi kununua.
Hii ni kanuni ya kuanza watu wachache, ambao utawatumia kama chambo kuwashawishi watu wengine kununua.
Kwa sababu, ukianza na watu wachache wanaofanya kitu na wengine pia wataiga.
Pale mteja anapokuwa na wasiwasi wa bidhaa au huduma, jua mteja huyo anataka uhakika. Na hapo ndiyo mahali ambapo silaha hii inapaswa kitumika.
Kwa mfano, unapaswa kumwambia mteja pale anapokuwa njia panda hajui afanye nini unamwambia, usiwe na wasiwasi watu wengi wanainunua sana hii bidhaa au huduma kwa sababu ni nzuri, imara au ni bora, chukua hii na utakuja kunishukuru baadaye kwa sababu watu wengi wanainunua.
Msaidie mteja wako kufanya maamuzi.
Pale mteja wako anapokuwa njia panda, hajui nini anataka msaidie kufanya maamuzi kwenye kile unachouza.
Kwa mfano, wewe unauza nguo za watoto, na dukani amekuja baba ambaye anataka kumnunulia mtoto wake wa kike na hajui hata achukue nguo gani.
Wewe kama muuzaji, unapaswa kumsaidia kufanya maamuzi kwa kumwambia, Sina uhakika kama itakufaa lakini watu wengi wanawanunulia watoto wao nguo hii kwa sababu ni nzuri. Mchukulie hii mtoto wako, inafanya kazi vizuri sana kwa sababu watu wengi wanainunua.
Toa ofa kwenye kile unachouza. Itawafanya wateja wengi waweze kuambiana wao kwa wao. Kwamba kwa fulani kuna OFA, na watu huwa wanapenda kufuata mkumbo, watashawishika kuja na kwako kwa sababu anaona watu wengi wanafanya hivyo.
Kwa sababu kwenye jamii tumeaminishwa kwambaz kile kinachofanywa na wengi ndiyo sahihi hivyo wengi watakuja.
Hapo utawashawishi kufanya mauzo ya ziada.
Kwa sababu watu huwa wanapenda kuigana, tumia hii silaha ya ushawishi ya kufuata mkumbo kuwashawishi wateja wako kununua zaidi.
Tumia shuhuda, watu wengi na kuonesha namna gani bidhaa au kile unachouza kinavyonunuliwa na wengi na yeye kununua ni kitu sahihi kufanya kwa sababu watu wengi wanafanya hivyo.
Hatua ya kuchukua leo; anza na watu wachache wanaofanya kitu na wengine wataiga kufanya hivyo.
Tumia hii mbinu kwenye kufanya mauzo kwa kutoa shuhuda, mifano, pale mtu anapokuwa na wasiwasi tumia hii silaha ya ushawishi ya kufuata mkumbo.
Kitu kimoja zaidi, silaha ya kufuata mkumbo huwa inafanya kazi vizuri sana kwa sababu watu wanafanya mambo kwa mazoea.
Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz