Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Leo tunakwenda kujifunza silaha ya sita ya ushawishi na ya mwisho kati ya silaha sita.
Leo ikiwa ni jumamosi ya ushawishi, kwenye jumamosi yetu ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Silaha yetu ya sita ni silaha ya UHABA yaani SCARCITY. Uhaba ni moja ya silaha ambazo kila mmoja wetu anaiijua na amekuwa anaitumia kwa namna moja au nyingine, hata kama hajui anaitumia.
Siyo mara yako ya kwanza kukutana na matangazo ya biashara mbalimbali ambayo yanakupa ukomo wa muda au kiwango unachoweza kununua.
Kwa mfano, msimu huu wa sikukuu, unaambiwa ukinunua kipindi hiki cha Christmas utapata ofa na mwisho wa ofa ni kabla ya Christmas na wewe unasukumwa kwenda kununua ili USIKOSE ofa hiyo.
Ukomo unatusukuma kuchukua hatua haraka kwa sababu asili ya binadamu huwa tunaogopa kupoteza kupata kitu fulani.
Unapoambiwa leo ni siku ya mwisho kupata kitu fulani, unasukumwa zaidi kukipata.
Unaambiwa vitu vimebaki vichache, unakazana ili usikose.
Uhaba unatumika sana na ni silaha ambayo inafanya kazi vizuri sana kwa sababu inatumia saikolojia yetu kutusukuma kufanya maamuzi kwa haraka bila hata ya kufikiri.
Kitu chochote kinachopewa uhaba, kinaonekana kina thamani zaidi. Hivyo wewe kama muuzaji unapaswa kuwashawishi wateja wako kununua kwa njia ya uhaba. Badala ya kumwambia mteja bidhaa ziko nyingi, mwambie zimebaki chache.
Kwa asili, vitu vyenye thamani huwa havipatikani, kwa urahisi, huwa tunavithamini zaidi.
Kama binadamu tumejifunza kuchukua hatua pale fursa ya kupata kitu cha thamani inapojitokeza kwa sababu tusipofanya hivyo tutakipoteza kitu hicho na watu wanaogopa kupoteza.
Kwa mteja wako, wewe kama muuzaji mtengenezee mazingira ya uhaba, iwe ni kwenye muda au idadi ya vitu anavyoweza kupata.
Kupoteza kunaumiza kuliko raha ya kupata.
Sisi binadamu huwa tunaongozwa kwa hisia mbili kufanya maamuzi.
Hisia hizo ni furaha na maumivu.
Huwa tunafanya kitu kama kinatupa furaha au kama kinatuondolea maumivu.
Hisia ya maumivu ina nguvu kubwa kuliko hisia ya kupata.
Tunaumia zaidi kwa kupoteza kuliko raha tunayoipata kwa kupata zaidi.
Silaha ya UHABA ina nguvu kwa sababu ya maamuzi ya mkato ambayo huwa tunayafanya.
Kwenye uhaba kwa sababu tumezoea vitu vya thamani vinapatikana kwa uhaba, basi tunajijengea maamuzi ya mkato kwamba kila chenye uhaba kina thamani kubwa.
Kwa mfano, unaweza kutoka nyumbani huna mpango wa kununua nguo, ukakutana na duka njiani la nguo wameandika punguzo la asilimia 50 , mwisho leo.
Kwa sentensi hiyo ya uhaba ,unajikuta unanaswa.
Kadiri kunavyokuwa na uhaba wa kitu , ndivyo tunavyokosa uhuru wa kuwa nacho na kukitumia.
Kiasili, sisi binadamu huwa hatupendi kupoteza uhuru ambao tunao na hivyo tunakimbilia kuchukua hatua ili tusipoteze uhuru huo.
Hivyo basi, kwenye uhuru tunasukumwa kuchukua hatua ili tusipoteze nafasi ya kukosa kitu hiko.
Uhaba unatusukuma kutaka zaidi.
Pale kitu kinapopatikana kwa uhaba, shauku yetu ya kuwa na kitu hicho inakuwa kubwa zaidi.
Hivyo basi, washawishi wateja wako kwa uhaba kwa sababu binadamu tunathamini kitu ambacho kina uhaba.
Kile ambacho kipo tu, huwa tunakipuuza kuchukua hatua haraka.
Chochote ambacho huwa kinapigwa marufuku kwenye nchi au jamii huwa kinapewa thamani zaidi na kanuni ya uhaba ndiyo inakuwa inafanya kazi. Kwa mfano, uhaba wa sukari, kupigwa marufuku kwa madawa ya kulevya.
Uhaba unatusukuma kutaka zaidi, kwa mfano, utafiti uliowahi kufanywa kwa wanafunzi wa chuo, ambapo walipewa tangazo la kitabu.
Wanafunzi hao waligawanywa kwenye makundi mawili.
Kundi la kwanza tangazo lilieleza ni riwaya ya mapenzi na kundi la pili tangazo lilieleza ni riwaya ya mapenzi kwa watu wazima tu, hairuhusiwi kwa wenye umri chini ya miaka 21.
Habari njema ni kwamba, walipofuatiliwa kujua ni wapi wana shauku kubwa ya kupata kitabu, wa kundi la pili, walikuwa na shauku kubwa kuliko kundi la kwanza.
Mpendwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, hapo umeona jinsi uhaba unavyoongeza thamani ya kitu, hata kabla ya mtu kukipata kitu hiko.
Hatua ya kuchukua leo; kwa chochote kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma unayotoa hakikisha unawasukuma watu kuchukua hatua kwa kutumia silaha hii ya uhaba.
Uza kwa uhaba na watu watachukua hatua na utakuja kunishukuru baadaye nenda kalifanyie kazi somo hili la leo kwa vitendo.
Kumbuka, HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Nenda kashawishi, ili uuze zaidi kila siku ya maisha yako kwa kutumia silaha ya UHABA.
Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz