Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Kusaka Wateja Kupitia Kuomba Rufaa.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya mauzo, eneo la usakaji. Haya ni masomo yanayotuwezesha kutafuta wateja tafajiwa wapya kwa wingi zaidi kwenye biashara zetu ili tuweze kukuza mauzo.

Kauli mbiu yetu ni; USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.

Ni kupitia kusaka ndiyo biashara inatengeneza wateja tarajiwa wengi zaidi. Na biashara yenye wateja tarajiwa wengi, haiwezi kushindwa kufanya mauzo makubwa kama watafuatiliwa vizuri.

Zipo njia nyingi za kupata wateja wapya tarajiwa kwenye biashara ambazo tunaendelea kujifunza. Lakini njia moja yenye nguvu kuliko njia nyingine zote ni KUOMBA RUFAA. Hapa unawaomba wateja ulionao wakupe wateja wengine, ambao ni watu wao wa karibu.

Rufaa ni njia ya mkato ya kutumia imani ya wengine kuaminika na watu ambao hawakujui. Unawatumia watu ambao tayari wanakujua na kukuamini, kukuunganisha na watu ambao hawakujui, lakini wao wanawajua. Ile imani ambao wanayo kwa watu wao, inatumika kukuamini na wewe pia.

Njia hii ina ushawishi mkubwa kwa sababu watu wanapata taarifa zako kutoka kwa watu wao wa karibu, ambao tayari wanawaamini na hivyo wanakuamini. Kwa kuwa wanawajua watu wao wa karibu na wanajua hawawezi kuwapa kitu kisicho na manufaa, wanakuamini kama unavyoaminika na wale ulionao.

Njia ya rufaa pia haina gharama kwa sababu huhitaji kuwalipa watu kuwaambia watu wao wa karibu kuhusu manufaa wanayopata kwako. Unaweza kuwapa zawadi wale wanaokuletea watu, lakini hiyo siyo gharama ukizingatia uhakika wa watu unaowapata.

Kwenye tasnia ya masoko, njia ya rufaa au ambayo kwa jina jingine inaitwa neno la mdomo (word of mouth) ndiyo njia namba moja na ya uhakika ya kuwafikia na kuwashawishi watu wapya.

Jinsi Ya Kuomba Na Kupata Wateja Wa Rufaa.

Ili kuweza kuomba na kupata wateja wapya tarajiwa kwa njia ya kupata rufaa kwa wateja waliopo kwenye biashara, fanyia kazi mambo yafuatayo.

1. Toa thamani kubwa na huduma bora.

Njia ya uhakika ya kupata pale unapoomba kitu chochote kile, ni kutangulia kwanza kutoa. Kwenye kuomba na kupata wateja wa rufaa, anza kwa kutoa thamani kubwa na huduma bora kwa wateja wako. Wafanye wateja wajione wakiwa na deni kwako kwa thamani na huduma waliyopata. Kwa kuwa watu huwa hawapendi kujiona wakiwa na deni, unapowaomba rufaa baada ya kuwa umewanufaisha sana, wanakuwa tayari kukupa.

2. Omba msaada.

Watu huwa wanapenda kutoa msaada pale wanapoombwa, hasa msaada huo unapokuwa ndani ya uwezo wao kuutoa. Unaweza kutumia njia ya kuomba msaada kupata wateja wa rufaa kwa uhakika. Unachofanya ni kuwaomba msaada wateja ambao tayari unao, wakupe watu wao wa karibu ambao nao wanaweza kunufaika na biashara yako kama ulivyonufaika wewe. Unapotumia njia hii, unatoa maelezo kabisa ya kuomba msaada. Unaanza kwa kuwauliza wateja kama wanaweza kukusaidia kitu kidogo. Hapo watakujibu ndiyo, kisha utawaomba wakupe mtu mmoja wa karibu kwao ambaye anaweza kunufaika na biashara yako. Kwa sababu walishakubali kukusaidia kitu kidogo na rufaa kuwa ni kitu kisichokuwa na gharama kwao, watakupa mtu au kukuahidi kukupa kama kwa wakati huo hawana.

3. Toa kadi maalumu.

Kuna wateja unaweza kuwahudumia vizuri, ukawaomba rufaa na wakawa tayari kukupa, ila wakati huo wakawa hawana mtu wanayemjua ambaye anaweza kuwa na uhitaji wa kile unachouza. Wateja hao watakuahidi vizuri kwamba wakikutana na mwenye uhitaji, watamleta kwako. Lakini tunajua maisha huwa yana mambo mengi, hivyo siyo mara zote wateja watakubali kutimiza kile walichokuahidi. Kuondokana na hali hiyo, unaweza kuandaa kadi maalumu za kuwapa wateja ambapo watawapa wale wenye uhitaji na kuja nazo kwako. Kadi hizo zinakuwa kitu cha kuwakumbusha kukuletea rufaa. Lakini pia kadi hizo zinaweza kutumika kutoa zawadi kwa wateja walioleta rufaa na zawadi kwa wateja waliokuja kwa rufaa.

4. Kuwa na msimamo kwenye thamani na ubora.

Kuna wateja wanaweza kuwa wananunua kwako, lakini ukiwaomba wakupe wateja wa rufaa wanakuwa hawapo tayari kufanya hivyo. Hiyo ni kwa sababu wanawajua watu wao hawataweza kuwa na uvumilivu kama walionao wao kwa thamani na huduma wanayoipata kwenye biashara yako. Biashara nyingi zimekuwa hazina msimamo kwenye thamani na ubora unaotolewa, kitu kinachofanya zisiweze kutegemewa na kuaminiwa. Kwa wewe kuwa na msimamo kwenye thamani na ubora, ambapo kila mteja anapokuja anapata thamani kubwa na ubora wa hali ya juu, anaamini na kuwa tayari kuwaleta wengine. Pia pale unapopewa rufaa na mteja, hudumia vizuri sana rufaa hiyo ili wale waliowaleta washukuriwe na waliokuja, kitu kinachowafanya wajisikie vizuri na kukuletea wengi zaidi.

5. Toa zawadi kwenye rufaa.

Watu wanapenda kupata zawadi, hivyo kwa wateja ulionao ambayo tayari wananufaika, unaweza kuwaahidi zawadi pale wanapokupa mteja wa rufaa na akanunua. Tenga aina ya zawadi au ofa utakayowapa na washawishi wakuletee wateja wa rufaa ili waweze kupata. Hapa unaweza kuweka mpango maalumu wa wateja kupata manufaa kwa kila mteja wa rufaa wanayemleta na akanunua. Kwa kuwa ni kitu ambacho hakiwaongezei gharama yoyote, huku kikiwa na manufaa, watashawishika kuchukua hatua. Kutekeleza njia hii utatumia kadi maalumu ambayo itamtambulisha mteja wa rufaa aliyekuja ametoka kwa nani ili aweze kupata zawadi yake. Kunaweza kuwa na njia nyingine za kutambua wateja walioletwa na wateja wengine ili wale waliowaleta wapate zawadi kama walivyoahidiwa.

6. Toa zawadi kwa rufaa.

Namba 5 ni kutoa zawadi kwa yule anayeleta mteja wa rufaa. Hii namba 6 ni kutoa zawadi kwa mteja anayekuja kwa rufaa. Hapa unaahidi zawadi, ofa au punguzo kwa wale wateja ambao wanakuja kwa njia ya rufaa. Hivyo unawaambia wateja ulionao kwamba kama wataleta wateja wa rufaa, basi wateja hao watapata zawadi au punguzo kwenye manunuzi watakayofanya. Watu watasukumwa kutumia njia hiyo kwa sababu wanataka kuwanufaisha watu wao wa karibu. Pia wanataka washukuriwe kwa jinsi ambavyo kupitia wao watu hao wa karibu wameweza kupata zawadi au punguzo. Pale mtu anapoenda kununua na kuambiwa anapata zawadi au punguzo kwa sababu ameletwa na mteja ambaye tayari yupo, anajisikia vizuri na atamshukuru yule aliyemleta. Njia hii pia inaambatana na matumizi ya kadi maalumu au njia nyingine ya kupima na kuthibitisha kweli mteja ametokana na njia ya rufaa na pia kumjua aliyetoa rufaa.

7. Toa rufaa kwa wengine.

Kwenye biashara na hata maisha kwa ujumla, mahusiano mengi yamejengwa kwenye nipe nikupe. Hivyo chochote ambacho unataka kupata, unapaswa kuanza kwa kuwapa wengine kwanza kitu hicho. Hivyo kwa wateja ambao tayari unao, tafuta rufaa unazoweza kuwapa. Kama nao wanauza, wape rufaa ya wateja wa uhakika. Au kama kuna vitu vingine wanavyonunua ambavyo wewe huuzi, wape rufaa za uhakika za mahali wanakoweza kununua. Kwa kumnufaisha mteja kwa rufaa unazompa, atakuwa tayari kukupa na wewe rufaa pia. Ni rahisi kuwapa wateja rufaa kama utakuwa unawahudumia vizuri na umewaelewa kwa undani na hilo litawafanya wao kukupa rufaa kwa uhakika pia.

8. Tumia shuhuda kupata rufaa.

Shuhuda ambazo wateja wanazitoa kwenye biashara yako, unaweza kuzitumia kama rufaa. Unachofanya ni kutumia ushuhuda kwa mtu ambaye anamjua. Kwa mfano unamshawishi mteja mpya anunue kwako, lakini hana imani kwa sababu hajawahi kununua. Lakini katika mazungumzo unagundua anajuana na mteja ambaye tayari unamuuzia na ameridhika. Hapo unaweza kutumia ushuhuda wa mteja huyo kumshawishi mteja kununua. Kama kuna ushuhuda ambao tayari ulishaandaa kutoka kwa mtu huyo unaweza kuutumia. Kama hakuna ushuhuda uliouandaa, unaweza kuwasiliana naye na kumwomba atoe ushuhuda kwa huyo mtu anayejuana naye. Kwa mteja kusikia kutoka kwa mtu anayemjua na kumwamini, anashawishika haraka zaidi. Hapa unakuwa umelazimisha rufaa wewe mwenyewe, kwa kumtumia mteja ambaye tayari unaye kuongea na mteja mwingine anayemjua. Hii ni njia nzuri kutumia pale unapokuwa na shuhuda za watu maarufu au wenye ushawishi kwa wengine. Unapotoa ushuhuda wa watu hao, wale wanaowajua wanautumia kama imani ya kununua kwako, kwa sababu wanayemwamini tayari ananunua kwako.

9. Kuuza kwa mfumo wa mtandao wa rufaa.

Kuna mfumo wa mauzo kwenye biashara ambao unatumia mtandao wa rufaa kama njia pekee ya kuuza bidhaa au huduma. Mfumo huu huwa unajulikana kama biashara ya mtandao (network marketing au multi level marketing). Kwa mfumo huu, mteja anashawishiwa kununua kitu, kisha akishanunua anakuwa ameingia kwenye mtandao na kila anapowashawishi watu wengine nao wakanunua, anapata kamisheni kupitia manunuzi ya watu hao aliowashawishi yeye. Kwa mfumo huu, mtu anaweza kuwatumia watu wake wa karibu kujiongezea kipato. Mfumo huu unafanya kazi vizuri pale bidhaa au huduma inayouzwa inakuwa na matumizi endelevu hivyo watu kuhitajika kununua mara kwa mara. Hata kama biashara yako haipo kwenye mfumo huu moja kwa moja, bado unaweza kutumia nguvu ya mtandao wa rufaa kupata wateja wa uhakika na watakaonunua kwa muda mrefu. Unachofanya ni kuwapa wateja mkakati wa kupata kamisheni kwa kila mteja wanayemshawishi kununua na kamisheni hiyo kuwa endelevu kila mara mteja huyo anaponunua tena. Kwa kuwa ni kazi ya mara moja ila yenye malipo endelevu, wateja watashawishika kufanya hivyo. Lakini pia njia hii itakusaidia kuwabakisha wateja kwenye biashara kwa muda mrefu, kwa sababu wataendelea kushawishiwa na wale waliowaleta, kwa sababu wanataka kuendelea kupata kamisheni kupitia manunuzi yao endelevu.

10. Omba rufaa kwa usahihi.

Moja ya sababu zinazowafanya wauzaji wengi kukosa wateja wa rufaa ni kutokuuliza kwa usahihi. Wengi wanaomba wateja wa rufaa kwa maswali ambayo yanaishia kujibiwa hapana. Kwa mfano wengi huwa wanawauliza wateja; Kuna mtu mwingine unayemjua ambaye anaweza kunufaika na biashara yetu kama unavyonufaika wewe? Swali la aina hiyo ni rahisi kujibiwa hapana na mteja. Na kwa sababu watu huwa wanapenda kufanya vitu rahisi, kwa swali hilo utapata majibu mengi ya hapana kuliko majibu ya ndiyo. Kuondokana na hali hiyo, unapaswa kuomba rufaa kwa usahihi, kwa kuuliza hivi; Nani mwingine unayemjua ambaye anaweza kunufaika na biashara yetu kama unavyonufaika wewe? Kwa kuwa swali limeanza na nani, moja kwa moja linampeleka mteja kwa watu anaowajia ili kuona yupi anaweza kunufaika kama yeye. Kwa swali hili la NANI utapata rufaa nyingi zaidi kuliko swali la KUNA. Omba rufaa kwa usahihi ili uweze kuzipata kwa wingi na ukuze wateja unaowauzia, kitu ambacho kitakuza zaidi mauzo kwenye biashara yako.

Fanyia kazi njia hizo za kuomba na kupata rufaa ili uweze kupata wateja wapya tarajiwa wengi zaidi kwa njia ya rufaa. Kwa kuwa njia ya rufaa ndiyo njia bora na yenye ushawishi, ni wajibu wa kila muuzaji kuitumia kupata wateja wapya tarajiwa.

Usakaji ndiyo pumzi ya biashara, unapaswa kufanyika mara zote.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

Leave a comment