Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Jinsi Ya Kupata Wateja Wengi Na Endelevu Kwenye Biashara Yako

Pata picha unatoka zako nyumbani, uko zako kwenye mishe mishe zako mara ghafla unakutana na mwanamke au mwanaume anakusalimia na kukuambia nimekupenda naomba nikuoe au unioe kwa mara ya kwanza tu na hamjawahi kuonana hata siku moja utajisikiaje kwa mfano?

Utamshangaa! vipi huyu kaka au dada amechanganyikiwa nini? Au atakua ana wazimu?

Au wewe ni mwanaume halafu kuna mwanamke unampenda, umemchunguza ukaona ni mtu sahihi kwako, kwa nini uendelee kuteseka roho na unaweza kumwambia? Basi unatoka na kwenda kumwambia, habari Asha, mimi naitwa Juma, nimekupenda naomba twende nikafunge ndoa na wewe leo. Je, unafikiri Asha atakubali? Je, kama ingekuwa wewe ndiyo Asha ungemkubalia Juma?

Au Juma anatoka na kumfuata Sikujua, anaenda kumtongoza Sikujua ili aweze kufunga naye ndoa. Juma anaenda kumueleza Sikujua hisia zake, jinsi gani anavyompenda na kumwitaji kuwa mke wake. Ile tu Juma anamalizia kumwambia Sikujua, hapo hapo Sikujua anamwambia basi sawa, twende tu tukafunge ndoa sasa hivi.

Kama wewe ndiyo Juma utamchukuliaje Sikujua? Utamshangaa kweli, ni mwanamke gani ambaye amekubali haraka hivi, atakua ana shida gani? Kwa nini akubali haraka hivi? Utakua na maswali mengi ambayo yatakufanya hata usitishe tena wazo lako la kumuoa Sikujua, kwa sababu ya jinsi alivyokubali kirahisi.

Mpendwa rafiki yangu, katika hali ya kawaida kwenye mifano hiyo hapo juu tuliyoiona, tuna kitu ambacho tunaweza kujifunza kwenye mchakato wa MAUZO.

Hata kama wewe uko kwenye mahusiano ya kimapenzi, mchumba, mke au mume uliye naye, hukumpata kwa siku moja. Ulitumia mchakato mrefu mpaka ukafanikiwa kumpata yule uliye naye sasa ambaye unamwita mke, mume au mchumba wako.

Kama ilivyo kuanzisha mahusiano ya kimapenzi ilivyokuwa mchakato. Vivyo hivyo, hata kuanzisha mahusiano ya kimauzo ilivyokuwa ni mchakato.

Ni wateja wachache sana ambao utawatafuta siku moja na wakanunua siku hiyo hiyo. Wengi watapenda kwanza mjenge mazoea, mahusiano, wakati mwingine wasiwasi wa kununua kwa mtu asiyemjua unamfanya mteja ajenge hali ya kutokuamini.

Lakini, kama mtu ni rafiki yako, amekuja na kukushawishi kununua huduma au bidhaa unayouza ni rahisi sana kukubaliana naye. Je, kwa nini ni rahisi kukubaliana naye? Kwa sababu tayari mko katika mahusiano ya kirafiki.

Wewe mwenyewe ukitaka kitu, lazima utauliza kwa watu wako wa karibu. Au mtu wako wa karibu, akikuambia sehemu fulani wanatoa huduma nzuri au wanauza kitu fulani, moja kwa moja utamwamini mtu wako wa karibu kuliko mtu mwingine.
Hata akija muuzaji wa hiyo bidhaa kukushawishi kununua unaweza hata usikubali lakini wewe utakapompendekezea rafiki, atakuamini na kuchukua hatua.

Sina uhakika kama itakufaa lakini, MAUZO NI MAHUSIANO. Utakua na mtazamo chanya kukubaliana na hili kwamba mauzo ni mahusiano kulingana na mifano ambayo tumeiona hapo juu?

Mauzo ni mahusiano kwa sababu tunanunua kwa watu ambao tunawajua.
Kila mmoja wetu akitaka kitu, hawezi kwenda kununua kwa mtu asiyemjua, kila mtu ana mtu wake kwenye huduma au kile anachotaka kununua hivyo akitaka bidhaa au huduma anaenda kwa mtu anayemjua.

Kama muuzaji, ni ngumu kumuuzia mtu ambaye bado hamjajenga naye mahusiano. Kumbe basi, ili uweze kumuuzia mtu kupitia huduma au bidhaa unayouza, ni lazima kwanza mjenge mahusiano ambayo yatafanya mauzo kuwa rahisi.

Mauzo yanakuwa magumu pale muuzaji anapotaka kumuuzia mtu kwa mara ya kwanza. Mauzo siyo tukio, mauzo ni mchakato na mchakato ndiyo unapelekea mauzo kuwa mahusiano.

Tunatengeneza mchakato wa mahusiano ya kimauzo ili mauzo yetu yaje kuwa rahisi. Kutaka kuuza kwa mteja ambaye unakutana naye kwa mara ya kwanza ni kama vile mfano ambao tuliona hapo juu wa Juma na Asha. Juma anataka kumuoa Asha kwa mara ya kwanza tu walivyoonana jinsi ilivyokuwa ngumu kwa Asha kukubali ndivyo ilivyo pia kwa mteja kukubali kuuziwa kwa mara ya kwanza na mtu ambaye hana mahusiano naye.

Kabla hujakimbilia kuuza huduma au bidhaa unayouza, hakikisha kwanza unajenga mahusiano na wateja wako tarajiwa.

Ukikutana na mteja kwa mara ya kwanza, wewe jenga naye kwanza mahusiano ya kirafiki, ukishamfanya mtu kuwa rafiki yako, ni rahisi kununua kwako. Kwa sababu, watu wananunua kwa watu ambao wanawajua. Kama mteja hakujui, ni ngumu kununua kwako.

Watu wananunua kwa watu ambao wanawapenda. Kama wateja hawakupendi, hawawezi kununua kwako. Na ili mteja akupende, lazima uwe umejenga naye mahusiano ya kiurafiki. Unapokuwa na urafiki na mteja, ataona wewe ni rafiki yake wa kweli, hivyo atakujali na kukupenda na kwa kuwa watu hawapendi kuwatesa watu ambao wanawapenda, hata ukimshawishi kununua, atanunua tu kwa sababu ya heshima ya urafiki ambayo umeijenga kwake.

Watu wananunua kwa watu ambao wana waaamini. Kama watu hawakuamini, wanakosa imani na wewe. Hivyo basi, ili watu wakuamini, sharti uwe umejenga nao mahusiano ya kiurafiki.

Ukijenga uaminifu kwa wateja wako, watakuamini bila shaka yoyote na hata kununua kwako. Imani ya mteja inajengwa kwenye uhakika, ukiwa na uhakika, wateja hawawezi kuwa na shaka na wewe.

Mauzo ni kazi ngumu kama ukiifanya kwa urahisi, na mauzo ni kazi rahisi kama ukiifanya kwa ugumu.

Sisi binadamu ni viumbe vya mahusiano, tunawaamini sana wale ambao tunahusiana nao kuliko wale ambao hatuhusiani nao. Kama ukiweza kuijua dhana hii ya MAUZO NI MAHUSIANO, basi ninakuhakikishia utaweza kuuza mpaka utashangaa wewe mwenyewe.

Habari njema ni kwamba, kitabu cha MAUZO NI MAHUSIANO, kipo jikoni, kinamaliziwa kupikwa, nawa mikono, chakula kinakuja mezani.

Je, unataka mbinu za ushawishi za kumteka mteja wako na kumfanya awe wako daima?

Je, unataka kuuza mpaka watu wakuone kama vile unatumia kizizi?

Je, unataka kuwa na wateja wengi wasiokuwa na ukomo wa kufanya manunuzi?

Je, unataka mbinu ambazo ukizitumia kwenye mauzo na kukusaidia pia kuboresha na kuimarisha mahusiano yako na mwenza wako?

Kama jibu lako ni ndiyo, nitumie ujumbe kwenda email au barua pepe makamu@mauzo.tz kwa kusema, Nataka kuwa mtu wa kwanza kukisoma na kuwekwa kwenye historia ya kitabu cha MAUZO NI MAHUSIANO.

Kitu kimoja zaidi, mauzo ni njia sahihi ya kuweza kupata chochote kile unachotaka kwenye maisha yako. Mauzo ndiyo ushindi wa uhakika, ukipata umepata, hivyo usipange kukosa kusoma kitabu hiko, siyo tu kitakusaidia sana kwenye mauzo, bali pia kuboresha mahusiano yako, utakuja kunishukuru baadaye baada ya kukisoma kitabu hiko.

Naomba unisaidie kitu kidogo, naomba unisaidie kuisambaza makala hii kwa mtu wako mmoja tu unayempenda ambaye unataka naye aje kunufaika kama utakavyonufaika wewe na kitabu cha MAUZO NI MAHUSIANO.

Kutoka kwa rafiki na muuzaji mwenzako,
CIO, Mwl Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa Chuo Cha Mauzo,
Barua pepe; makamu@mauzo.tz
Simu; 0717101505 wasapu na kawaida/0767101504.
http://www.t.me/chuochamauzo
www.mauzo.tz

Leave a comment