Habari za leo ndugu yangu mpendwa? Naamini umewahi kuona nyumba ikiungua moto, simu ikiishiwa vocha, nguo ikichanika, Kingamuzi kikiishiwa kifurushi, maji yakikatika au gari likiishiwa mafuta. Ni hali za kawaida kutokea katika maisha yetu.
Je, nyumba ilipoungua ulienda kwa nani kupata usaidizi?
Simu ilipoishiwa vocha ulienda kununua wapi?
Nguo ilipochanika ulienda kwa nani ili kuirekebisha? Kadhalika na vitu vingine. Kuna sehemu sahihi ulienda kupata utatuzi.
Kama ni nyumba, kuungua. Ulienda kupata usaidizi zimamoto na uokozi. Simu ilipoishiwa vocha ulienda duka kununua vocha. Nguo ilipochanika ulienda kwa fundi cherehani ili airekebishe. Kadhalika na sehemu zingine.
Lakini kama ingetokea nguo ikachanika ukaenda duka la dawa usingepata utatuzi wa tatizo lako. Au kama nyumba ilivyoungua ukaenda hospitalini usingepata utatuzi wa tatizo lako. Bali ungeendelea kuangaika. Kilichofanya uende sehemu husika ni kwa sababu ulikuwa unajua huduma wanayotoa.
Hali ya namna hiyo ipo katika biashara au huduma tunazotoa. Bila kumjua mteja unayemhudumia, itakuwa ngumu kuona kama ameridhika au unampatia utatuzi wa tatizo lake.
Unapomhudumia vizuri anafurahia huduma yako. Hili ndilo eneo muhimu kufanyia kazi kama mhudumiaji au muuzaji unayetaka kukuza huduma yako. Ni vema kumjua mteja wako.
Zipo namna nyingi za kumjua mteja wako. Leo tunaangalia moja pekee. Namna yenyewe ipo kwenye TATIZO UNALOTATUA.
Unachopaswa kujua ni kuwa, kila mtu anayeishi katika ulimwengu huu kuna tatizo anakabiliana nalo. Iwe anajua au hajui, lakini lipo tatizo analo. Kuwa na nyumba tayari ni tatizo. Simu, vifaa vya mawasiliano, chakula, mavazi yote hayo ni matatizo amebeba tayari.
Ni wewe tu kuchagua eneo moja wapo na kuanza kulifanyia kazi. Linaweza kuwa eneo la afya, chakula, mavazi, nafaka, ujenzi au usafiri. Unapoanza kufanyia kazi kitu hicho wateja watajua na kufuata.
Japo sio wote watakufuata. Ila ukifanya kwa msimamo utawafikia wengi. Kitu muhimu unachopaswa kuhakikisha unafanya ni biashara yako kumjua mteja. Maana bila kumjua mteja utajikuta unatumia nguvu kubwa kuwahudumia hata wasiohusika. Tuchukulie mfano, unauza dawa unaangaika na mtu ambaye gari lake limepata changamoto anahitaji fundi alitengeneze.
Kumjua mteja inakusaidia kujua namna gani unapaswa kuongeza nguvu ya kumshawishi kulingana na mahitaji yake. Ukisha mjua mteja unatakiwa kujenga mahusiano mazuri naye. Kwa sababu malengo makuu ya biashara ni kujenga ukaribu na mteja pamoja na kumjali mteja.
Eneo hilo ukilifanyia kazi vizuri utaweza kuwajua watu wengi wenye mahitaji na kuwasaidia. Nikuhakikishie kuwa, hakuna kitu utafanya na kukosa wateja hakuna kabisa. Maana kila mtu lipo tatizo anakumbana nalo katika muda asiotarajia.
Unatatua tatizo kupitia huduma yako. Na hiyo ndiyo dhana ya mauzo ni huduma. Mahali popote alipo binadamu lipo tatizo amebeba.
Je, umewahi kuisikia google?
Je, unatumia Google kutafuta vitu vyako?
Jibu lipo wazi. Kila mmoja anapotaka kujua kitu au kutafuta kitu, sehemu ya kwanza kuingia ni “Google”. Anaingia na kuandika hitaji chake. Hapo hapo anapata majibu. Tena anapata majibu zaidi ya vile anavyodhania.
Unaweza kuuliza jinsi ya kuongeza mauzo, ukapata maelezo mengine ya kina mbinu na namna zipi unaweza kutumia kukuza mauzo. Pia, unaweza kukutana na vitabu husika katika eneo la mauzo.
Usichujua kuhusu Google ni kitu kimoja, sio kwamba wao wanaandika kile unachotaka. Bali walikusanya taarifa nyingi zaidi na kuziweka katika mtandao wao.
Hivyo, unapokuwa umeandika kitu ikiwa kipo moja kwa moja wanakuletea kama ilivyo. Ikiwa hicho kitu hamna watakuletea makala za watu tofauti tofauti zinazoelekeana na ulichouliza. Wanaamini ukipata mwanga unaweza kupata majibu ya tatizo lako. Inapaswa kuwa hivyo katika huduma yako. Unaweza kukusanya taarifa nyingi za wateja na kuona namna gani unazitumia kuwasaidia kupata huduma.
Google inalenga “search” na ndilo tatizo wanalotatua. Kumbe, ili kumjua mteja wako lazima ujue tatizo unalotatua. Wateja wako watakuja kutafuta suluhu.
Google waliweka nguvu kuleta suluhu juu ya swali lolote linaloulizwa kupitia ukurasa wao. Wameleta mapinduzi makubwa katika utafutaji wa vitu, kwa sababu sio rahisi utafute kitu ukikose. Watu wameweka nguvu na uaminifu mkubwa kwao. Maana ni taarifa nyingi muhimu wanazipata kutoka kwao. Naamini hata wewe umewahi na unaendelea kutafuta vitu kupitia ukurasa wa huo.
Hebu tupate sifa kidogo za Google
Moja. Uharaka.
Unapotafuta kitu hawachelewi kukuhudumia. Kama upo katika sehemu yenye mtandao mzuri utatumia sekunde chache kupata majibu ya swali lako.
Mbili Usahihi.
Unapotafuta kitu, wanakupa kitu chenyewe kilivyo, kisha kukuwekea taarifa zingine zinazoelekea au kufanana. Ukisoma taarifa zote hukosi kupata jibu sahihi.
Tatu. Uelewa.
Ni rahisi kuelewa taarifa zao maana wanaleta nyingi kuhusiana na kitu unachotaka. Huenda mbali na kuweka lugha tofauti ili wewe mwenyewe uchague ipi unataka kutumia. Wanaenda zaidi ya matarajio.Unapotafuta kitu, hawakupi na kuishia hapo. Wanakuletea vitu zaidi ya kumi. Ni wewe kuchagua wapi uangalie kulingana na matakwa yako.
Nne. Unafuu wa gharama.
Huhitaji kuwa na gharama kubwa kutafuta kitu chako. Hata kama bando lako ni dogo una uhakika wa kupata taarifa nyingi unazotaka.
Je, biashara au huduma yako inatatua tatizo lipi?
Muhimu; Biashara yako haipaswi kuwa tatizo, bali chanzo cha suluhu. Wateja wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ni wewe kuja na suluhu juu ya changamoto hizo. Rejea kwenye mfano wa Google namna inavyotatua matatizo ya wateja wake. Kisha jifanyie tathmini wewe na biashara au huduma yako uone namna ya kujiboresha zaidi.
Ukitoa huduma bora na kutatua changamoto au matatizo ya watu. Biashara au huduma yako itakua zaidi. Weka akilini kuwa haupo pale kujifurahisha, upo unatoa huduma. Hivyo, mauzo unapaswa kuyachukulia kama sehemu ya huduma. Wahudumie vema wateja wako, wataipenda biashara au huduma yako.
Umeweka mkakati upi kuhakikisha biashara yako inawajua wateja wake? Shirikisha hapa hapa tujifunze zaidi.
Twendeni tukatoe huduma bora kwa wateja wetu.
Habari njema ni kuwa, kitabu cha MAUZO NI HUDUMA kipo jikoni kinapikwa. Ni wewe kukaa mkao wa kula kukipokea kitakapokuwa tayari. Lengo ni kukuza ufahamu upande wa mauzo na kuyakuza zaidi.
Imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tujifunze zaidi. Tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata kitabu na kujifunza zaidi.
Mauzo ni huduma
Hide comments