Je, wajua kuwa, unaweza kumuuzia mteja kwa urahisi na haraka?
Fuatilia somo hili utapata mbinu zaidi;
Maria na Jenifer wanauza duka katika eneo A. Wote wanauza bidhaa zinazofanana. Yaani; Rosheni, mikoba na pochi za wanawake. Bei zao hazitofautiani, maana wote “Supplier” wao ni mmoja. Maria anauza zaidi kuliko Jenifer. Kila unapofika mwisho wa mwezi na wakati wa kuagiza mizigo, Jenifer anapata taabu. Kwa sababu pesa kwake inakuwa inapungua kuliko Maria.
Jenifer sio mtu wa starehe kusema pesa zake zinatumika vibaya, anao utulivu mzuri na anaijua vema pesa. Mara zote anaitumia katika masuala ya msingi. Je, unafikiri tatizo lipo wapi? Kwanini Maria auze zaidi kuliko Jenifer?
Ni maswali mengi unaweza kujiuliza, labda kuna mchezo unafanyika, wanatofautiana kwenye muda wa kufungua duka na mengine mengi, lakini huo sio ukweli.
Jenifer na Maria ni marafiki, hawajawahi kugombania wateja, kiujumla wanasaidiana sana. Kila mmoja anamsaidia mwenzake pale anapokwama. Kinachofanya Maria kuuza zaidi ni uwezo wake wa kumshawishi mteja kununua. Hilo ndilo jibu la swali letu.
Unachopaswa kujua ni kwamba, ili mteja anunue lazima ushawishi vema. Uzuri wa ushawishi haupo tu kwenye mauzo, upo katika sehemu zote. Kiongozi anayepenya kwenye siasa lazima awe na uwezo mzuri kuwashawishi watu.
Je, unafanyaje ili kumshawishi mteja ili umuuzie kwa urahisi?
Kitu kimoja katika mengi ya kumshawishi nayo ni kumfanya mteja aongee.
Hakuna kitu kigumu kwenye kutoa huduma, kama kukutana na mtu asiye ongea. Ni ngumu kiasi kwamba unashindwa namna gani umsaidie. Shida kubwa inapoanzia ni unaanzia wapi kumuhudumia.
Kama mtu hajakwambia hitaji lake sio rahisi kukadilia. Hii ni kwa sababu, “siri ya moyo haijuaye kifua, na moyo wa mtu hausomeki”. Sio rahisi umtazame mtu usoni na kujua mahitaji yake. Ingekuwa hivyo, basi tungeaibika. Maana, kuna muda pesa inatuishia hadi tunatia huruma. Lakini mtu bila kuongea, huwezi kujua nini anataka au changamoto aliyonayo. Ni kupitia kuongea, ndipo unaweza kujua mahitaji yake.
Unajua kwanini matapeli wanatuibia? Ni kupitia kutuongelesha ndipo tunajikuta tumeishaibiwa. Wanaanza kutusalimia tunaitikia, baada ya hapo maswali mawili matatu. Baadaye tunanogewa, tunajikuta stori zishaanza kuwa nyingi. Inapofika pointi wanata kufanya yao, bila sisi kujua tunajikuta kiulaini tunaibiwa.
Yote hiyo ni kwa sababu tuliruhusu kuongea nao. Ikiwa huongei, hamna mtu anaweza au lolote linaweza kukuzuru. Maana kunakuwa hakuna mlango wa kuingiza mada ya mazungumzo.
Unapoenda kununua kitu huwezi kufika na kumpatia pesa mhudumiaji akakupa bidhaa unayotaka. Lazima uongee, kupitia kuongea ndipo anajua kile unachokitaka.
Ipo hivyo kwako muuzaji, unapotaka kumnasa vizuri mteja wako na kumshawishi, kitu cha kwanza kabisa mfanye aongee kwa hali yoyote ile. Hapo tayari utakuwa na mahali pa kuanzia.
Je, ili kumfanya mteja aongee, ufanye nini? Usiwe na wasi, nimeandaa makala hii kwa ajili yako. Haya hapa mambo ya kuzingatia;
Mosi; Mpe salamu.
Habari njema ni kwamba, salamu sio kitu kipya au kigeni kwetu. Hasa waafrika. Mtu anapotusalimia huwa ni rahisi kumwitikia. Kitendo cha mtu kukuitikia, ni ishara ameruhusu na kufungua mjadala wa mazungumzo. Ikiwa mtu hana muda na wewe mara nyingi anaweza asisikie hata salamu yako.
Kijana anapotaka kumtongoza binti, kitu cha kwanza kwake huwa ni salamu. Kitendo binti kuitikia salamu ni fursa kwa kijana kuongeza neno jingine.
Kadiri binti anavyozidi kuitikia ndivyo anavyozidi kunogewa. Kinachofuata baada ya hapo namba ya simu au miadi. Hivyo hadi anafanikisha kutoa yaliyo moyoni.
Hata wewe kuendelea kuwashawishi wateja wako anza hivyo, kadiri mtu anavyokupa nafasi nenda naye hadi mwisho.
Pili; Zungumzia kitu chochote kulingana na mazingira mliyopo.
Hapa namaanisha, angalia vitu vilivyowazunguka. Kisha chagua kitu kimoja, jifanye kama unamuuliza. Ikiwa mteja yupo katika biashara yake, angalia ukubwa au bidhaa zilizopo chagua moja uizungumzie au msifie kwa kuwa nayo. Au kama una watoto, mke au mume wake au amevaa jezi ya timu yoyote. Hapo ni pazuri pa kuanzia. Kumbuka tunataka aongee.
Sio kwa ulazima mtu aongee na wewe lakini kwenye kutoa huduma kuongea kuna nguvu kubwa sana. Ni sawa na daktari anapotaka kukupatia huduma lazima akufanye uongee ndipo ajue wapi anatibu. Huwezi kufika mbele yake naye akasema basi chukua panado au mseto utakua sawa. Lazima uongee ndipo aone namna ya kukupa tiba.
Kwenye biashara yako tiba ni huduma unayotoa. Ongea na mteja umhudumie. Wakati ndio huu kuongeza ushawishi kwa wateja wako ili uuze zaidi.
Je, wajua kwamba kumshawishi mteja akajisikia vizuri ni sehemu ya huduma bora? Ndiyo. Habari njema ni kuwa, kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA kipo jikoni kinaandaliwa. Njia nyingine za kumshawishi mteja zipo ndani ya kitabu hicho. Endelea kutufuatilia hapa hapa ili uwe wa kwanza kupata kitabu hicho pindi kitakapokuwa tayari.
Imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata makala na kitabu.
Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze zaidi
Hide comments