Ndugu, Chukulia mfano huu, mtu anataka kukupa laki moja ya ziada, anakupa shilingi uirushe hewani. Utachagua upande utajitokeza juu, iwe ni kichwa au mkia. Ukirusha shilingi hiyo na upande uliochagua ukijitokeza juu, anakupa laki moja. Lakini kama utarusha shilingi hiyo na upande utakaojitokeza juu ukawa tofauti na ule uliochagua basi wewe utapaswa kutoa laki moja.
Je, utakubali kucheza mchezo huo? Jibu lipo wazi ni hapana. Unataka kujua kwa nini? Kwa sababu maumivu ya kupoteza laki moja uliyonayo ni makubwa kuliko raha ya kupata laki moja nyingine.
Ndivyo ilivyo kwa wateja tunaokutana nao katika biashara yetu. Kile kinachomfanya mteja kufika katika eneo lako ni kitu kinachomuumiza zaidi.
Hakuna mtu anaweza kuacha maduka au sehemu zingine zote na kuja kwako bila kuwa na uhitaji wa kitu. Labda wewe ushindwe tu kuongea naye na kujua kinachomsibu. Mfano mwingine, tuchukulie mtu anayeumwa labda malaria au kichwa. Ili apate suluhisho anapaswa kwenda hospitali au duka la dawa.
Ili uweze kumshawishi mtu huyo kununua, unapaswa kujua maumivu aliyonayo na kuyagusa hayo wakati unazungumza naye. Maumivu huwa yanajificha nyuma ya hisia anazokuwa nazo mtu. Kwa kuzijua hisia hizo kwa mteja na kuzitumia, unakuwa umegusa maumivu yake na kuweza kuwashawishi kununua.
Kwa mtu anayeumwa kichwa au malaria lazima atakuwa anaongea kwa unyonge sana, kazi kwako muuzaji kumsikiliza na kumuuliza maswali. Bila kujua hasa nini kinamuumiza akili hutoweza kumshawishi kununua.
Sisi binadamu huwa ni viumbe wa kihisia zaidi, tunapenda kujiona kwamba tunafanya maamuzi yetu kwa kufikiri kwa kina. Lakini huo sio kweli, huwa tunafanya maamuzi yetu kwa hisia na kuyahalalisha baadaye.
Kama mtu unakipenda kitu, utakikubali kwanza, halafu ndiyo utaanza kuangalia sababu za kukikubali. Kama hutaki kitu, utakikataa kisha kutafuta sababu za kukikataa.
Kama muuzaji unayetaka kumjua mteja, hili ni jambo muhimu sana unalopaswa kulijua sio tu kwenye mauzo, bali kwenye maeneo yote ya maisha yako. Pale unapotaka kuwashawishi mtu, anza kwa kugusa hisia zake.
Ndiyo maana mtu anapotaka kukuibia huwa anaanza kuteka hisia zako. Anakwambia ukilipa hii utapata hiki ndani ya muda mfupi utakuwa umepata pesa nyingi zaidi. Kwa kuwa pesa ni eneo linaloleta msisimko mkubwa mtu unapolisikia unajaa. Unapojaa unakuwa na uwezo mkubwa kukushawishi na kukuibia pesa zako. Ukweli ni kwamba hisia zikiwa juu kiwango cha maamuzi sahihi kinakuwa kipo chini.
Ndiyo maana Dale Carnegie aliwahi kusema: “Kuna njia moja pekee ya kumshawishi mtu afanye kitu chochote. Njia hiyo ni kumfanya atake kufanya kitu hicho. Kumbuka hakuna njia nyingine.” Njia hiyo ni kumpa kitu anachotaka. Huo ndiyo msingi mkuu wa kuwashawishi watu wafanye chochote kile, kwa kuwafanya wao wenyewe watake kufanya kitu hicho.
Na njia ya kuwafanya watu watake kufanya kitu chochote kile ni kugusa hisia zao. Kwa kuwa watu hufanya maamuzi kwa hisia, unapogusa hisia sahihi kwa watu, unawafanya wao wenyewe watake kufanya kitu, ili wapate wanachotaka au wasipoteze walichonacho.
Wateja wanokuja kwako kuna pesa wanayo, ili usipoteze ongelea maumivu na kugusa hisia zao. Kama nilivyoandika hapo awali. Kila mteja anayekuja kwako muone kama anayo laki na zaidi ameileta katika biashara yako. Kila akiondoka hujamuuzia jua laki moja umeipoteza. Je, upo tayari kuendelea kuipoteza? Jibu ni hapana. Gusa maumivu na hisia zake, hii itakuchochea kuwahudumia vema zaidi.
Je, ni mara ngapi umekuwa ukiwapoteza wateja kisa hujagusa maumivu yao?
Habari Njema Ni Kwamba Kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA kipo tayari Hardcopy. Ndani yake kimeelezea mengi kuhusu namna ya kugusa maumivu na kuteka hisia za wateja ili uwashawishi zaidi. Ni wewe tu kuchukua kitabu hicho kwa ajili ya kupata maarifa zaidi.
Makala imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata makala na kitabu.
Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi.
Hide comments