Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Tofauti ya silaha za ushawishi na silaha nyingine ni kutokuhitaji matumizi ya nguvu au mabavu.
Kwa mfano, kama unataka kuwalazimisha watu wafanye kitu fulani, unaweza kutumia nguvu lakini, hiyo inakuwa na gharama na madhara yake.
Sina uhakika kama itakufaa lakini, kwa kutumia silaha za ushawishi huhitaji nguvu yoyote. Ni wewe tu kugusa njia ya mkato iliyo ndani yao na kuwaacha wao wakitekeleza wenyewe.
Silaha ya kulipa fadhila yaani Reciprocation ni mbinu kuu ambayo imekuwa inatumiwa na wale wanaotaka kupata kitu kutoka kwa watu wengine, ni kwa kuanza kuwapa watu kitu kwanza.
Pale unapopewa kitu na mtu, anakuwa ametengeneza deni kwako na hivyo unakuwa umesukumwa kulipa fadhila.
Pale mtu huyo aliyekupa kitu anapokuja na ombi kwako, unakubaliana naye.
Kifupi, silaha hii ni silaha ya kutengeneza madeni ambayo mtu analazimika kuja kukulipa baadaye.
Ni silaha ambayo unamwachia mtu hatia ndani yake. Usipomrudishia wewe mwenyewe unakuwa unaumia ndani yako. Na kwa kuwa watu hawapendi kujisikia vibaya, wanajikuta wanalipa tu fadhila.
Hii ni silaha inayogusa kanuni ya kijamii ambayo inaeleza kwamba tunapaswa kulipa wema ambao wengine wametufanyia.
Kwa mfano, mtu akikupa zawadi, basi na wewe mpe zawadi.
Mtu akikusaidia unapokuwa na uhitaji, na wewe msaidie atakapokuwa na uhitaji.
Kwa mfano, wauza karanga, wanatumia mbinu hii ya kulipa fadhila. Wanakuonjesha karanga bure kabisa kisha baadaye unashawishika kuja kununua. Unakuwa unaona tayari amekupa hivyo na wewe unawajibika kwenda kununua karanga. Anakuwa kama ametengeneza deni kwako.
Sasa tunatumiaje kanuni hii kuweza kuuza zaidi kwenye biashara zetu?
Tunatumia silaha hii kama kutengeneza madeni kwa wateja wetu, kutengeneza madeni ni kutengeneza mazingira ya wateja kuja kununua kwetu.
Ili umpate samaki, lazima umtengenezee chambo ambayo itakusaidia kumnasa kirahisi.
Unapaswa kutengeneza madeni kwa wateja wako kwa njia zifuatazo;
Moja, ukipata nafasi ya kumhudumia mtu, mpe huduma bora kiasi cha kufurahia huduma au bidhaa yako na kutaka kurudi tena.
Kila mtu anapenda huduma bora, hivyo wape watu huduma bora ndiyo njia ya kutengeneza madeni mengi kwa wateja wako na baadaye watakuja kununua kwa kulipa fadhila kwa sababu ya uliwapa huduma bora.
Mbili, wasaidie wateja kupata kile wanachotaka. Kwa njia ya kutoa maudhui, elimu elimishi. Unapotoa elimu elimishi juu ya kitu unachouza siku wanapokuwa na uhitaji hawataenda sehemu nyingine zaidi ya kwako kwa sababu tayari ulishatengeneza deni kwao.
Tatu, wafanye wateja wasijikie vizuri kuja kwako. Kwa njia ya kuwasifia familia yake, kuweka maoni kwenye _status’ zao walizoweka. Hii inawafanya unawajali na wao watajisikia vizuri.
Wakijisikia vizuri, tayari utakua umetengeneza deni ambalo watapaswa kulilipa kwa njia ya kununua kile unachouza.
Nne, kama bidhaa au huduma yako unayotoa inaweza kuonjeshwa, waonjeshe ili kutengeneza deni na kuja kulipa fadhila.
Kwa mfano kwenye bidhaa kama vile karanga, maziwa nk.
Na kwenye huduma kama vile kumpatia mwezi mmoja au wiki bure na baada ya ofa hiyo mshawishi huduma unayotoa na atakuwa tayari kununua.
Hatua ya kuchukua;
Toa kwanza ili uweze kupokea.
Tengeneza madeni ili uweze kulipwa.
Kutoa ni uwekezaji. Wekeza kwa wateja wako.
Mwisho,tumejengewa katika jamii kwamba, mtu akikusaidia na wewe unapaswa kumsaidia.
Hivyo basi, hakikisha kwenye biashara yako unawateka wateja wengi zaidi kwa kuwasaidia kwenye kile wanachotaka ili na wewe upate kile unachotaka.
Kumbuka watu ni wabinafsi, wanapenda unajali mambo yao, jali mambo yao na wao watajali kuhusu biashara yako.
Kauli mbiu yetu ni HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz