Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.
Usakaji ni kitu kinachopaswa kufanyika kwa uendelevu kwenye mauzo.
Siyo kitu cha kufanya na kuacha, bali ni kitu cha kufanya bila ya ukomo.
Wakati msakaji au muuzaji anapokuwa na wateja wachache anaowafuatilia, huwa ni rahisi kwake kuwakumbuka wateja hao kwa taarifa zao na miadi yao mbalimbali.
Lakini kadiri muda unavyokwenda na wateja kuwa wengi, kuwakumbuka wote inakuwa siyo rahisi.
Na hapo ndipo changamoto nyingi zinapozaliwa, zinazotokana na wateja kusahaulika.
Njia ya kuondokana na changamoto hiyo ya wateja kusahaulika ni matumizi ya mfumo wa kutunza taarifa na kumbukumbu za wateja.
Mfumo huo huwa unajulikana kwa kifupi kama CRM, ambapo kirefu chake ni Customer Relationships Management.
Kwa Kiswahili rahisi ni mfumo wa kufuatilia wateja.
Faida za kutumia CRM.
Mfumo wa CRM una manufaa mengi kwenye mauzo, hapa tutaangalia makubwa matatu.
Moja ndiyo Kanzidata (Database) kuu ya wateja kwenye biashara.
Hapa taarifa zote za wateja zinatunzwa vizuri. Kuanzia majina, mawasiliano, tarehe muhimu kwao na hata vitu wanavyopendelea.
Kadiri taarifa nyingi zaidi za wateja zinavyojulikana, ndivyo inavyokuwa rahisi zaidi kuwashawishi.
Ni muhimu taarifa zote za wateja zitunzwe vizuri ili zisisahaulike na pia ziweze kutumika pale zinapohitajika.
Mbili ndiyo sehemu ya kutunza kumbukumbu za ufuatiliaji wa wateja.
Chukua mfano umewapigia simu wateja 50 leo na 20 kati yao wakakuambia uwatafute mwisho wa mwezi, ambao ni kama wiki mbili zijazo.
Unadhani ni wangapi kati ya hao 20 utakumbuka kuwatafuta?
Na hata wale ambao utakumbuka kuwatafuta, unadhani ni wangapi utakumbuka mazungumzo mliyofanya wiki mbili zilizopita?
Wakati wa kufanya tukio, unaweza kuona ni rahisi kukumbuka.
Lakini muda unavyokwenda ndiyo unagundua jinsi ilivyo vigumu kukumbuka.
Hapo ndipo mfumo wa CRM unapokuwa na manufaa kwenye mauzo.
Kwa kuweka vizuri kumbukumbu za ufuatiliaji unaofanya kwa wateja, unakukumbusha wakati wa kuwafuatilia tena.
Na kabla ya kuwafuatilia tena, unapitia mazungumzo ya nyuma na kujua mwendelezo wa kwenda nao.
Tatu ndiyo njia nzuri ya kuwachuja wateja kabla ya kuwafuatilia.
Wasakaji na wauzaji wengi wamekuwa hawapati matokeo mazuri kwenye kufuatilia wateja wao kwa sababu wanakosa mpango mzuri.
Wanapoianza siku yao ya mauzo, wanaanza kushambulia kila mteja anayekuwa mbele yao.
Kinachotokea ni wanakutana na wateja ambao bado ni wa baridi sana na hivyo kutokupata matokeo mazuri.
Hilo linawakatisha tamaa na kuona ufuatiliaji wanaoufanya hauna maana.
Lakini kama mtu atachukua hatua ya kuwachuja wateja kabla ya kuwafuatilia, atajua wale ambao wapo karibu zaidi na kufanya maamuzi na kuanza kuwafuatilia hao kwanza.
Kwa kuanza na wateja wa aina hiyo, inakuwa rahisi kwao kupata ushindi ambao unawapa hamasa ya kuendelea zaidi.
Taarifa zilizopo kwenye mfumo wa CRM ndiyo zitakuongoza wateja wapi ambao wapo karibu zaidi na kufanya maamuzi.
Kwa manufaa hayo na mengine mengi, tunaona ni muhimu kwa kila mtu anayejihusisha na mauzo kutumia mfumo wa CRM ili kufanya mauzo yake vizuri.
Ugumu wa wengi kutumia CRM.
Licha ya manufaa makubwa ya kutumia CRM ambayo tumeyaona, bado wasakaji na wauzaji wengi wamekuwa wagumu kutumia zana hiyo vizuri.
Sababu kubwa ya kukwama kutumia mfumo huo ni mtazamo hasi wanaokuwa nao kwamba kutumia CRM ni kujiongezea kazi ya ziada.
Kwa sababu CRM inamtaka mtu kuingia kwenye mfumo na kuandika maelezo ya ufuatiliaji uliofanyika kwa kila mteja, wengi huona ni kupoteza muda.
Lakini ukweli ni muda unaotumia kuweka taarifa za ufuatiliaji wa wateja kwenye CRM siyo muda unaopoteza bali ni muda unaowekeza kufanya mauzo kuwa rahisi zaidi baadaye.
Ni sawa na mkata mti ambaye anatumia muda kunoa shoka lake kila baada ya ukataji wa muda fulani.
Wasioelewa wataona kunoa shoka ni kupoteza muda, lakini shoka ambalo ni kali litakata mti kwa muda mfupi zaidi kuliko shoka butu.
Wewe usiwe na mtazamo hasi ambao wasakaji na wauzaji wengine wanao.
Wewe penda na kubali kutumia mfumo wa CRM kwenye mchakato wako wa mauzo kwa kuzingatia yafuatayo;
- Andikisha wateja wako wote kwenye mfumo wa CRM. Na kadiri unavyoendelea kupata taarifa zaidi za wateja wako, endelea kuzitunza kwenye mfumo huo.
- Kwa kila ufuatiliaji unaoufanya kwa wateja wako, tunza kumbukumbu zake kwenye mfumo wa CRM. Kama kuna ahadi zimewekwa, ziingize kwenye mfumo ili kukumbushwa pale muda unapofika.
- Andika maelezo ya ufuatiliaji vizuri na kwa usahihi na kuyaweka kwenye CRM. Usiandike tu hovyo hovyo ili kumaliza kwa haraka. Kumbuka unachoingiza ndiyo utakachotoa. Ukiingiza uchafu, unatoa uchafu.
- Kabla ya kumfuatilia mteja, ingia kwenye mfumo wa CRM na pitia ufuatiliaji uliofanyika nyuma ili kukumbuka na kuwa na mahali pazuri pa kuanzia. Hiyo inasaidia usiwe unaanza upya kila wakati.
- Usitafute njia rahisi wala ya mkato kwenye matumizi ya CRM. Pita njia iliyo sahihi kwa sababu huo ni uwekezaji muhimu kwenye kukuza mauzo yako.
Mfumo wa MAUZO.TZ CRM
Kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO, mfumo wa CRM tunaoutumia ni wa MAUZO.TZ.
Mfumo huu umetengenezwa kuendana na programu yetu, hasa kwenye taarifa muhimu za wateja tunazohitaji katika kuwafuatilia.
Na kikubwa zaidi ni hatua za ufuatiliaji za kuhakikisha tunamgusa kila mteja kwa njia mbalimbali zisizopungua 10 bila ya kumchosha, kabla hatujamkatia tamaa kwamba siyo mnunuaji.
Mfumo wa MAUZO.TZ CRM una sifa zote za CRM kama tulivyojifunza na umeenda hatua za ziada kwenye kuhakikisha taarifa zote muhimu za ufuatiliaji wa wateja zinawekwa kwa usahihi.
Yafuatayo ni mambo ya ziada yaliyopo kwenye mfumo wa MAUZO.TZ CRM ambayo hayapatikani kwenye mifumo mingine ya CRM;
- Namba kuu 10 za mchakato wa mauzo ambazo zinagusa kila eneo la mauzo na kuwezesha mauzo makubwa kufanyika.
- Hatua maalumu za ufuatiliaji ambazo zinapaswa kufanyika kwa kila mteja kabla ya kumkatia tamaa.
- Malengo ya ufuatiliaji kuwekwa na ripoti kujitengeneza zenyewe kulingana na ufuatiliaji unaofanyika.
- Majukumu ya kufanya (To Do List) kutengenezwa na muda wa kukamilisha. Pia ahadi za wateja kujitokeza moja kwa moja kwenye majukumu kwenye tarehe ya kutekeleza.
- Ufuatiliaji kwenye kutembelea kuchukua eneo ambalo mtu yupo na hivyo kuondoa udanganyifu kwenye kutembelea.
- Kuweza kufanya mawasiliano ya moja kwa moja kutoka kwenye mfumo, kama kupiga simu, kutuma sms, barua pepe na mawasiliano mengine kama Whattsapp.
Kwa sifa hizo za kipekee na nyingine nyingi, mfumo wa MAUZO.TZ CRM ni wa muhimu kutumiwa kwa usahihi ili kuweza kuwafuatilia vizuri wateja na kukuza zaidi mauzo.
Jinsi ya kutumia MAUZO.TZ CRM
Ili kuweza kutumia kwa usahihi mfumo wa MAUZO.TZ CRM na kunufaika nao, kuna video za maelekezo rahisi.
Angalia video hizo kwenye channel ya Telegram ya mchakato wa mauzo.
Kuingia kwenye channel hiyo, BONYEZA MAANDISHI HAYA.
Angalia video kwa umakini kisha fanya hatua kwa hatua. Unapokwama rudi tena kwenye video.
Na pale unapokwama zaidi, tumia mawasiliano ya msaada yaliyopo kwenye mfumo huo wa MAUZO.TZ CRM ili kusaidiwa.
Kama unataka kufanya mauzo makubwa, lazima uwafuatilie wateja wako kwa ukaribu na umakini.
Kila ufuatiliaji unaofanya kwa wateja unapaswa kutunza vizuri kumbukumbu zake.
Tumia mfumo wa MAUZO.TZ CRM kutekeleza hilo.
Matumizi ya CRM ni ya muhimu kwenye hatua zote za mauzo, kuanzia usakaji, ukamilishaji, uhudumiaji na ufuatiliaji. Hivyo ni sehemu muhimu ya mchakato wa mauzo.
Usakaji ndiyo pumzi ya biashara, unapaswa kufanyika mara zote.
Kocha Dr. Makirita Amani,
Mkuu wa CHUO CHA MAUZO
www.mauzo.tz