Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea,
Karibu tena katika jumatano yetu ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.
Baada ya kujifunza kwa kina kuhusu hatua za mauzo, vikwazo na sheria za kuzingatia, sasa tunakwenda kujifunza njia za uhakika za kukamilisha mauzo.
Hizi ni njia ambazo zimefanyiwa tafiti na zimekuwa zinatumiwa na wakamilishaji wenye mafanikio makubwa.
Usizisome tu njia hizi, bali zitafakari kwa kina, ziweke kwa mifano inayoendana na biashara yako kisha zifanyie mazoezi mpaka uweze kuzitumia kwa uhakika bila hata ya kusoma mahali.
Karibu ujifunze na kufanyia kazi njia hizi za uhakika za kukamilisha mauzo.
1. Ukamilishaji wa kupeleka.
“Lini unataka kuletewa ___ yako? Sasa hivi au kesho saa nne asubuhi?”
Kwa mfano, unadhania mteja anataka kitu fulani kwa kumwambia, lini unataka kuletewa pikipiki yako? Sasa hivi au kesho saa nne asubuhi.
Hapa unakuwa tayari umedhania kama mteja anataka na kama kweli anataka atakuambia. Ni njia ya kumpima mteja kama kweli anataka kile unachomuuzia au la.
Ni njia ambayo inamsaidia mteja kufanya maamuzi ya haraka.
Badala ya kumuuliza mteja kama unachukua au huchukui muulize kwa njia ya kudhania.
Chukulia bidhaa unayouza tayari mteja ana uhitaji nayo na kisha muulize lini apelekewe sasa hivi au baadaye na siyo kumuuliza je unachukua au huchukui.
Ukimuuliza mteja kama unachukua au huchukui ni swali ambalo linampa nafasi mteja kuwa na machaguo mawili ya kukataa au kukubali.
Ufafanuzi; Njia hii inadhania mteja ameshakubali kununua, kitu kinachofanya mteja akubali. Kamwe usimuulize mteja kama atachukua au hatachukua, muulize lini atachukua.
Na unapouliza, mpe umiliki kwa kutumia neno ‘yako’.
2. Ukamilishaji wa kuhakikisha.
“Je kuna mabadiliko mengine unayotaka kufanya kwenye _ yako kabla hatujaenda kwenye makubaliano ya bei?”
Kwa mfano, unamwambia mteja je, kuna mabadiliko mengine unayotaka kufanya kwenye hii oda yako,( una taja bidhaa yako au huduma unayotoa ) kabla hujaenda kwenye makubaliano ya bei?
Ufafanuzi; njia hii inadhania umiliki, inaondoa kukataliwa na kutengeneza fursa ya kukamilisha mauzo.
Pale mtu unapomuuliza kama kuna mabadiliko na kukuambia hakuna, kinachofuata baada ya hapo ni kumwambia mteja akamilishe malipo ili aondoke na bidhaa yake.
Unapotumia njia hizi, jiamini, kuwa na uso wa tabasamu, shauku kubwa. Na mteja akishaonesha nia ya kutaka kitu, hapo hapo mkamilishe kwa kutumia mbinu hizi mbili ulizojifunza leo.
Hatua ya kuchukua leo; nenda kazifanyie kazi njia hizi mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo kisha uje ushuhudie matokeo uliyapata.
Kumbuka mauzo ni vita.
Lakini, ni vita isiyoruhusu kumwaga damu.
Pambana ili ushinde, uko vitani na usipouza basi utauziwa.
Kazi yako wewe ni kuuza na siyo kuuziwa.
Kuuza ni pale unapopokea fedha kutoka kwa mteja na kuuziwa ni pale unapopewa sababu na mteja na kukuacha bila kufanya mauzo.
Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz