Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Mkakati Mkuu Wa Usakaji Endelevu Kwenye Chuo Cha Mauzo.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.

Kikwazo cha kwanza kwenye mauzo na ukuaji wa biashara ni wateja kutokujua kuhusu uwepo wa biashara.

Unaweza kuwa na bidhaa au huduma nzuri sana na ya thamani.
Lakini kama wateja unaowalenga hawajui kuhusu uwepo wa kile unachouza, hutaweza kufanya mauzo makubwa.

Ndiyo maana usakaji ndiyo hatua ya kwanza na muhimu kufanyia kazi ili kukuza mauzo kwenye biashara.

Na usakaji siyo kitu cha kufanya mara moja na kuacha.
Bali ni kitu cha kufanya kila mara, kama tu upo kwenye biashara, unapaswa kuwa unafanya usakaji kwa msimamo na uendelevu.

Usitumie matokeo unayopata kuacha usakaji, bali yatumie kuboresha usakaji.
Usiache usakaji kwa sababu unapata matokeo madogo, bali boresha usakaji wako.
Pia usibweteke kwenye usakaji pale matokeo yanapokuwa makubwa, bali endelea kufanya kwa ukubwa zaidi.

Kwa kuwa msimamo kwenye ufanyaji wa kitu chochote ndiyo eneo ambalo wengi wanakwama, programu yetu ya CHUO CHA MAUZO ina mkakati mkuu wa usakaji ambao unapaswa kufanyiwa kazi na watu wote.

Mkakati huo una vipengele vikuu vitatu;

Moja ni usakaji kufanyika kwa msimamo na mara zote bila kuacha, bila kujali ni matokeo gani yanapatikana.
Hapa kinachofanyika ni kuboresha kadiri unavyoendelea kwenda.

Mbili ni kila biashara kuwa na njia yake kuu moja ya usakaji ambayo ndiyo inafanyiwa kazi kwa ukubwa.
Njia nyingine pia zitatumika, lakini ile iliyo kuu itafanyiwa kazi kwa nguvu na ukubwa zaidi.

Tatu ni kila msakaji kuwafikia wateja wasiopungua 100 kwenye kila siku ya biashara. Hao ni wale wateja ambao wameguswa moja kwa moja na msakaji, wakajua kuhusu uwepo wa biashara kwa uhakika.
Mkakati wa kufikia wateja wasiopungua 100 kwenye kila siku ya biashara unapaswa kufanyiwa kazi na watu wote waliopo kwenye mauzo kwenye biashara, hata kama siyo wasakaji.
Kama mtu anafanya usakaji na ukamilishaji au utuatiliaji, bado atahitajika kuwafikia wateja wasiopungua 100 kila siku ya biashara.

Huu ndiyo mkakati mkuu ambao kila aliyepo kwenye programu ya CHUO CHA MAUZO analazimika kuufanyia kazi kwa uhakika.
Muhimu ni usiseme ni ngumu au haiwezekani, bali unapaswa kufanya kwanza kisha kwenda ukiboresha mpaka kuweza kukamilisha.

Njia kuu za usakaji.

Tumeona kila biashara kuwa na njia kuu moja ya usakaji ambayo inafanyiwa kazi kwa ukubwa.
Zipo njia nyingi za usakaji, kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO, tuna njia hizi kuu;

  1. Kuomba rufaa kwa wateja ambao tayari wapo kwenye biashara.
  2. Kuwatembelea wateja kule walipo, ambao hawaijui biashara au hawajawahi kununua.
  3. Kuwapigia simu wateja, ambao hawaijui biashara au hawajawahi kununua.
  4. Kutuma jumbe mbalimbali, za simu, mitandao na barua pepe.
  5. Kutoa maudhui mbalimbali na kwa njia mbalimbali.
  6. Kutumia mitandao ya kijamii na mikusanyiko mingine inayowaleta watu pamoja.
  7. Kutumia matangazo ya kulipia kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Katika njia hizi kuu, kila biashara na kila msakaji lazima achague njia yake kuu ambayo ndiyo ataitumia kwa ukubwa sana na uhakika.

Hesabu ya kuwafikia wateja 100 kwa siku.

Kwenye kuhesabu kuwafikia wateja wasiopungua 100 kila siku, haya ndiyo yatakayozingatiwa.

  1. Rufaa; zile ambazo zimefikiwa, yaani umeomba rufaa, ukapewa na kumfikia.
  2. Kutembelea; waliofikiwa, yaani umefika na kukutana na mteja. Simu; ulioongea nao, yaani umepiga simu, ikapokelewa na ukaongea na mtu.
  3. Jumbe (sms, emal, DM); zilizojibiwa, yaani umetuma ujumbe na mtu akakujibu. Kama umetuma jumbe 100, wakajibu 20, uliowafikia ni 20 na siyo 100.
  4. Maudhui; walioweka maoni/kujibu, yaani waliochukua hatua na kuandika kitu na siyo waliosoma (views) au waliopendezwa (likes).
  5. Matangazo; waliochukua hatua iliyoelekezwa kwenye tangazo na siyo walioona au kusikia tangazo. Kama tangazo linasema mtu apige simu, limeonekana na watu 100 lakini 30 ndiyo wamepiga simu, hao 30 ndiyo wamefikiwa.

Ni rahisi kufikia namba 100 kwa siku.

Unaposikia kufikia wateja wasiopungua 100 kila siku, kitu cha kwanza utakachofikiria ni haiwezekani.

Lakini huo siyo ukweli, inawezekana sana.
Unachohitaji ni kuchanganya hizo njia za kuwafikia wateja.
Kwa mfano kupiga simu, kutuma jumbe, kutoa maudhui na kulipia matangazo.
Ukifanya zaidi ya kimoja kwenye siku, inakuwa rahisi kufikia hiyo namba 100.

Karibu tukae kwenye huu mkakati mkuu wa Usakaji kwenye programu ya CHUO CHA MAUZO ili tuhakikishe biashara zetu zinawafikia wateja tunaowalenga na kufanya mauzo makubwa.

Usakaji ndiyo pumzi ya biashara, unapaswa kufanyika mara zote.
Kocha Dr. Makirita Amani,
Mkuu wa CHUO CHA MAUZO
www.mauzo.tz

5 Comments

  • Lackius Robert
    Posted November 7, 2023 at 4:42 am

    Hongera sana Kocha Dr. Makirita Aman kwa somo zuri kuhusu usakaji. Hakika ni pumzi ya biashara ukifanyika kwa msimamo bila kuacha. Asante sana.

    • mauzo
      Posted November 7, 2023 at 1:50 pm

      Hakika Mkufunzi Lackius, bila hii pumzi biashara zitazorota na kufa.

  • Kizito bakwanye
    Posted November 7, 2023 at 7:13 am

    Asante kocha njia zangu kuu ambayzo nimezichagua kwenye usakaji ni kuomba rufaa nakupiga simu

    • mauzo
      Posted November 7, 2023 at 1:51 pm

      Vizuri, tumia njia hizo kwa uhakika.

  • Miraji abdallah
    Posted November 7, 2023 at 4:12 pm

    Nilichojifunza hapa ni inawazekana kabisa kufanya usakaji na ukawafikia wateja 100 kwa siku Kama tu utatumia njia tofauti tofauti Kama vile matangazo, maudhui, simu, rufaa na kadhalika.
    Kitu ninachoenda kufanya ni kujifunza njia nyingi za kuwafikia wateja pia kuzifanyia mazoezi ili iwe rahisi kuzitekeleza.

Leave a comment