Utembeleaji wa wateja, hiki ni kitendo cha kuwafikia wateja mahali wapo. Yaani, kufika katika biashara zao na kuona namna wanavyoziendesha. Unakuwa ana kwa ana na wateja.
Baadhi yetu tunajifariji kwa kusema; nimempigia simu, nimemtumia ujumbe au zawadi, basi inatosha. Sikia rafiki, kitendo cha kukutana na mtu ana kwa ana kina nguvu kubwa katika kumfanya mteja ajisikie vizuri. Hii ni kwa sababu anaona umemjali kwa kiwango cha hali ya juu. Maana kutembelea kunahitaji maandalizi na gharama pia. Vyote hivyo mteja anaviangalia.
Ni kweli tupo katika zama za sayansi na teknolojia ambapo tunasema “dunia ni kijiji”. Unaweza kumuona mtu unayeongea naye au kumpigia muda wote. Lakini kumbuka haupo katika biashara yake muda huo.
Kitu kimoja cha kujiuliza je, ni wauzaji wangapi wanampigia simu? Je, unafikiri simu yako itakuwa na upekee upi kwa mteja? Na vipi kuhusu ujumbe mfupi? Wangapi wanamtumia?
Ili uwe muuzaji bora kuwahi kutokea lazima ukubali kuingia gharama za kuwafuatilia wateja wako kwa njia ya utembeleaji. Huko utagundua vitu vingi pamoja na kutengeneza upekee kwa mteja kama nilivyoelezea hapa chini;
Moja, Kumjua wateja kwa kina.
Mteja anapokupigia atakwambia nipo sehemu fulani nauza hiki na kile naomba unitumie vifaa hivi imeisha. Lakini unapomtembelea katika biashara yake, utagundua kuna vitu huwa hanunui kwako. Hii ni sababu hajui kama unavyo. Au huwa ananunua kwa kiwango cha chini kulingana na biashara yake.
Mbili, Fursa ya kumuuzia vitu vingine. Mteja anapokupigia simu anakuelezea mahitaji ya muda huo. Pia, hupati nafasi ya kujua vitu vingine anavyouza. Lakini unapomtembelea unapata fursa ya kumpendezea vitu vingine kulingana na biashara au huduma yake.
Tatu, Kujenga uaminifu na mahusiano.
Sio kitu kilichozoeleka kwa wauzaji wengi kuwatembelea wateja wao. Hivyo, unapofanya hivyo mteja anaona kweli umeshamilia. Imani yake kuhusu biashara au huduma yako inaongezeka kwa kiwango cha hali ya juu.
Nne, kupata taarifa nyingi za mteja. Kwa njia zingine za ufuatiliaji inaweza kuwa ngumu kupata taarifa za mteja. Lakini unapomtembelea unazipata. Mfano umekuta amevaa jezi ya Simba unajua mnyama huyu. Akiwa na jezi ya Yanga unajua huyu mwananchi. Ukakutana na watoto au mke wake au nyumba na taarifa zingine zaidi unazokuwa umezipata kutoka kwake zinazoenda kukusaidia baadaye wakati wa ufuatiliaji.
Tano, Kutengeneza wateja tarajiwa wengi pamoja na rufaa.
Unapomtembelea mteja, unaweza kukuta pembeni yake kuna wauzaji wengine unaoweza kuwahudumia. Au ukamuomba rufaa akakupa na kuwaona kama wapo karibu. Ukiwa na baadhi ya bidhaa wakaziona ni rahisi kulipia. Unakuwa umewapunguzia mwendo wa safari kuzifuata mahali zilipo. Pia, inafanya wakujue zaidi. Maana wanakuwa hawakujui wala hawaijui biashara.
Uzuri wa njia hii ya utembeleaji unaweza kuonyesha shauku yako, ushawishi wako pamoja na kumsifia mteja kulingana na unavyomkuta. Ni njia inayosadikika kuwa na nguvu zaidi katika mauzo.
Maana inakupa nafasi ya kumwonyesha mteja mfano au kujaribu kitu. Hali inayoongeza ushawishi kwa mteja. Ni wewe tu kuchagua kitu unachoenda nacho au namna ya kumwingia mteja.
Ili uweze kuongeza kipato zaidi acha kujifungia sehemu moja kwamba lazima nipige simu, kutuma ujumbe tu bali fuatilia wateja kwa njia ya utembeleaji.
Kwa hayo pamoja na mengine mengi usikose kuchukua kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA. Ndani yake kimeelezea hatua kwa hatua jinsi ya kuwafuatilia wateja wako kwa ukaribu na kuongeza ushawishi.
Makala imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz
Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi
Karibuni.