Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Wateja tarajiwa wapo wengi zaidi.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Tumepata fursa nyingine ya kushirikishana masomo ya Usakaji.
Haya ni masomo yanayotuwezesha kutafuta wateja tafajiwa wapya kwa wingi zaidi kwenye biashara zetu ili tuweze kukuza mauzo.

USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.
Hiyo ndiyo kauli mbiu yetu ya usakaji ambayo tunaiishi na kuifanyia kazi.
Ni kupitia usakaji ndiyo tunaingiza wateja wapya kwenye biashara na hao ndiyo wanaoleta ukuaji mkubwa.

Kwenye somo hili tunakwenda kujenga na kuimarisha mtazamo mpya juu ya wateja tarajiwa ili tuondoe vikwazo vyote vya ukuaji kwenye mauzo na biashara.
Hapa tunakwenda kuona jinsi ambavyo wateja tarajiwa ni wengi na wanaendelea kuzaliwa kila siku hivyo hatuwezi kuwa na uhaba wa wateja kama tutafanya kazi yetu kwa uhakika.

Nilipokuwa mtoto, nilikulia eneo ambalo kulikuwa na watu wengi waliofanya kazi ya kuongoza watalii kupanda mlima Kilimanjaro.
Watu hawa waliporudi kutoka kwenye safari ya kuongoza watalii, walikuwa na fedha nyingi na ambazo walizitumia kwa anasa sana.
Walipokuwa wanaingia kwenye baa, walikuwa wanawanunulia watu pombe.
Pale walipokuwa wanaulizwa kuhusu matumizi yao ya fedha kwa kufuja, walikuwa na kauli ya kuwaambia watu hivi; “Hebu toka hapo nje uangalie kama mlima upo, kama mlima upo basi kazi zipo na fedha zipo.”

Japokuwa hawakuwa sahihi sana kwa hiyo kauli, siyo upande wa fedha, bali upande wa kazi, kwa sababu kazi zao zilikuwa za msimu na kipindi ambacho hakukuwa na kazi maisha yao yalikuwa magumu kwa sababu hawakuwa na akiba za kuwatosha.
Lakini kuna kitu kimoja nimependa kuhusu kauli hiyo, ile hali ya uhakika wa uwepo wa kazi, kwa sababu ya uwepo wa zana kuu ya kazi.

Hiyo ni kauli ambayo sisi wauzaji tunapaswa kujijengea kwa namna ambayo ni sahihi na kuitumia kukuza zaidi mauzo.
Na kauli yetu ni hii; WATEJA TARAJIWA WAPO WENGI ZAIDI.
Tulishajifunza jinsi ambavyo kikwazo cha kwanza cha ukuaji wa mauzo ni kukosekana kwa wateja wapya tarajiwa.

Mwaka 2022 nchi ya Tanzania ilifanya sensa ya watu na makazi.
Baadaye matokeo ya sensa hiyo yalitangazwa, yakionyesha kukiwa na ongezeko la idadi ya watu.
Wakati watu wengine wakielezea ongezeko hilo kwa namna tofauti tofauti, mimi nilisema na kurudia kauli hii; tuna wateja wengi zaidi wa vitu ambavyo tunauza.

Kama muuzaji, unapaswa kufurahia pale panapokuwa na ongezeko la watu, iwe ni kwa kuzaliwa au kuhamia.
Kwa sababu hao ni wateja tarajiwa wapya ambao wanakupa fursa ya kukuza mauzo yako na biashara kwa ujumla.

Huo ni upande mmoja wa kuiangakia kauli ya wateja tarajiwa wapo wengi, kwa uhalisia wake kupitia ongezeko la watu.

Upande wa pili wa kauli WATEJA TARAJIWA WAPO WENGI ZAIDI ni njia ya kukuza zaidi mauzo.
Kila unapokwama kufikia malengo yako ya mauzo, jua ni kwa sababu una wateja wachache na/au wateja hao hawafanyi manunuzi ya kutosha.

Hivyo hatua ya kwanza kabisa ya kuchukua ili kukuza mauzo ni kutengeneza wateja tarajiwa wapya kwa wingi zaidi.

Kama unakwamishwa na wateja ambao wanakuahidi watanunua halafu hawatimizi ahadi hizo, tatizo siyo hao wateja wanaovunja ahadi.
Bali tatizo ni wewe ambaye umeweka matumaini yako yote kwa wateja wachache wakati tarajiwa wapo wengi zaidi.

Kama umefuatilia wateja wote ulionao na bado ukashindwa kufanya mauzo makubwa, tatizo linaanzia kwenye uchache wa wateja ulionao. Ukiongeza wateja, ufuatiliaji wako pia utazaa matunda mazuri.

Kama ukiweka juhudi za kufuatilia zaidi wateja unaonekana kuwakera wateja kwa sababu unajikuta unawatafuta wateja wale wale kila mara, ni kwa sababu wateja ulionao ni wachache.
Hilo ni tatizo lako kwa sababu wateja tarajiwa wapo wengi zaidi, lakini wewe umeganda kwa wachache na hivyo kujikwamisha.

Kama mabadiliko ya kiuchumi, kimazingira au kimsimu yanaathiri mauzo yako kwa kiasi kikubwa, jua lawama za kwanza ni kwako mwenyewe.
Uliridhika na wateja uliokuwa nao ambao walikupa mauzo makubwa mambo yalipokuwa mazuri.
Lakini mambo yanapoyumba kwa hao wateja wachache, na kwako yanayumba pia.
Kama ungekuwa na wateja wengi zaidi, kuyumba kwa wateja wachache kusingeathiri mauzo yako kwa ukubwa.

WATEJA TARAJIWA WAPO WENGI ZAIDI ni kauli ya kutupa moyo, matumaini na msukumo wa kutokuridhika na wateja tulionao sasa.
Bali kuhakikisha kila wakati tunasaka na kutengeneza wateja wapya tarajiwa wengi zaidi kwenye biashara zetu.

Tunapoona watoto wanazaliwa, tufurahi ni wateja wapya tarajiwa wanaongezeka.
Tunapoona ongezeko la watu, tufurahie ni wateja wapya tarajiwa.
Na pale tunapokutana na watu ambao hawajui kile tunachouza, tufurahi ni fursa ya kuwajulisha na kuwashawishi wawe wateja.

Haijalishi biashara yako ina wateja wengi kiasi gani na inafanya mauzo makubwa kiasi gani, zoezi la kusaka wateja wapya tarajiwa halipaswi kuacha kufanyika.
Hilo ni zoezi linalopaswa kufanywa kwa uendelevu na msimamo bila kuachwa.
Kwa sababu ndiyo zoezi la kwanza na la msingi kwenye ukauji wa biashara yoyote ile.

Kila unapokuwa unapitia magumu kwenye mauzo na biashara kwa ujumla jiambie kauli hii kwa kujiamini; WATEJA TARAJIWA WAPO WENGI ZAIDI.
Kisha anzia hapo, kwa kufikia wateja wapya tarajiwa wengi zaidi na kuwaingiza kwenye mchakato wa kuwafuatilia na kuwageuza kuwa wateja kamili wa biashara yako.

Kwenye mauzo na biashara huwezi kufa njaa kama unao wateja wengi wanaonunua kwako na unaowahudumia vizuri.
Na kwa sababu watu wanazidi kuongezeka, wateja tarajiwa pia wanaongezeka na hiyo kuwa fursa nzuri kwako muuzaji kuwa na wateja wengi na kufanya mauzo makubwa.

Kila wakati fikia wateja tarajiwa wengi na waweke kwenye mchakato wa kuwafanya wateja kamili, hiyo ndiyo njia ya ukakika ya kukuza mauzo na biashara kwa ujumla. Na uhakika ni; WATEJA TARAJIWA WAPO WENGI ZAIDI.

Usakaji ndiyo pumzi ya biashara, unapaswa kufanyika mara zote.
Kocha Dr. Makirita Amani,
Mkuu wa CHUO CHA MAUZO
www.mauzo.tz

2 Comments

  • Faraji
    Posted November 28, 2023 at 5:55 am

    Ni kweli usakaji makini bila kuchoka itasaidia kampuni

  • Miraji abdallah
    Posted November 28, 2023 at 8:25 pm

    _kama unafuatilia wateja ,lakini mauzo yako chini,
    _kama Kufuatilia wateja unaona unawakera,
    _na pia mabadiliko ya kiuchumi ,maz
    ingira yakuathili basi sababu ni wewe.
    Ili kutoka ktk mkwamo huo
    HAKIKISHA zoezo la kusaka wateja wapya tarajiwa linakuwa endelevu, changamoto zote hizo zinasababishwa na uchache wa wateja.

Leave a comment